Date: 
30-01-2023
Reading: 
Yohana 9:13-23

Jumatatu asubuhi tarehe 30.01.2023

Yohana 9:13-23

[13]Basi wakampeleka kwa Mafarisayo yule aliyekuwa kipofu zamani.

[14]Nayo ilikuwa sabato, hapo Yesu alipofanya zile tope na kumfumbua macho.

[15]Basi Mafarisayo nao wakamwuliza tena jinsi gani alivyopata kuona. Akawaambia, Alinitia tope juu ya macho, nami nikanawa, na sasa naona.

[16]Basi baadhi ya Mafarisayo wakasema, Mtu huyo hakutoka kwa Mungu, kwa sababu haishiki sabato. Wengine wakasema, Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya ishara kama hizo? Kukawa matengano kati yao.

[17]Basi wakamwambia yule kipofu mara ya pili, Wewe wasemaje katika habari zake kwa vile alivyokufumbua macho? Akasema, Ni nabii.

[18]Basi Wayahudi hawakusadiki habari zake, ya kuwa alikuwa kipofu, kisha akapata kuona; hata walipowaita wazazi wake yule aliyepata kuona.

[19]Wakawauliza wakisema, Huyu ndiye mwana wenu, ambaye mnasema kwamba alizaliwa kipofu? Amepataje, basi, kuona sasa?

[20]Wazazi wake wakawajibu, wakasema, Tunajua ya kuwa huyu ndiye mwana wetu, tena ya kuwa alizaliwa kipofu;

[21]lakini jinsi aonavyo sasa hatujui; wala hatujui ni nani aliyemfumbua macho. Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima; atajisemea mwenyewe.

[22]Wazazi wake waliyasema hayo kwa sababu waliwaogopa Wayahudi; kwa maana Wayahudi walikuwa wamekwisha kuafikiana kwamba mtu akimkiri kuwa ni Kristo, atatengwa na sinagogi.

[23]Ndiyo sababu wale wazazi wake walisema, Ni mtu mzima, mwulizeni yeye.

Kung'aa kwa Yesu Kristo;

Sura nzima ya 9 katika Injili ya Yohana inamhusu mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa, jinsi alivyoponywa na Yesu kwa kupakwa tope usoni. Katika somo la asubuhi hii, Mafarisayo wanauchunguza uponyaji wa Yesu kwa kipofu. Hawakuamini uponyaji ule. Walimuuliza aliyeponywa kuhusu uponyaji ule, alipomkiri Yesu katika maelezo yake wakamtoa nje.

Tatizo ni kuwa Mafarisayo hawakuamini. Wao walisema wanamwamini Musa. Walipomtoa aliyeponywa nje, walimuuliza Yesu kuhusu nafasi yao kiroho, kwa kutokuamini kwao Yesu akawaita vipofu;

Yohana 9:40-41

[40]Baadhi ya Mafarisayo waliokuwapo pamoja naye wakasikia hayo, wakamwambia, Je! Sisi nasi tu vipofu?
[41]Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa.

Yesu aliwaambia dhahiri Mafarisayo kuwa ni vipofu. Hii ni kwa sababu hawakumuamini, hadi wakawa wanahoji huduma yake. Uponyaji ule ulikuwa ishara ya uwezo wa Yesu kama mponyaji. Kutomwamini Yesu kunatufanya kuwa sawa na Mafarisayo ambao hawakumwamini. Kutompokea Yesu kunatufanya kuwa vipofu rohoni. Tusichunguze habari za Yesu, bali tumwamini na kumwomba atuondolee upofu, yaani dhambi zetu. 

Uwe na wiki njema.