Date: 
09-05-2022
Reading: 
Yohana 1:43-51

Yohana 1:43-51
43 Siku ya pili yake alitaka kuondoka kwenda Galilaya, naye akamwona Filipo. Yesu akamwambia, Nifuate.
44 Naye Filipo alikuwa mtu wa Bethsaida, mwenyeji wa mji wa Andrea na Petro.
45 Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti.
46 Nathanaeli akamwambia, Laweza neno jema kutoka Nazareti? Filipo akamwambia, Njoo uone.
47 Basi Yesu akamwona Nathanaeli anakuja kwake, akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake.
48 Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona.
49 Nathanaeli akamjibu, Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli.
50 Yesu akajibu, akamwambia, Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya.
51 Akamwambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.

Maisha mapya ndani ya Yesu;

Yesu anamuita Filipo amfuate, Filipo naye anampa Nathanaeli ujumbe wa Kristo Mnazareti aliyetabiriwa na manabii. Nathanaeli anakuja kwa Yesu akimkiri kama mwokozi wa ulimwengu, lakini Yesu kumbe alikwishamtambua Nathanaeli tangu mwanzo, hata Nathanaeli mwenyewe akashangaa!

Ndivyo ilivyo, kwamba Yesu anatuona, anatufahamu. Hakuna jambo tunaloweza kumficha. Kama alivyomuita Filipo, anatuita nasi leo kumfuata katika maisha yetu ya imani. Tunapomfuata Yesu maisha yetu yanakuwa mapya.
Huu ndiyo wito wa Yesu kwetu, kwamba tutengeneze njia zetu, ili maisha yetu yawe mapya siku zote.
Tunakutakia wiki njema yenye maisha mapya ndani ya Yesu Kristo.