Date: 
27-01-2023
Reading: 
Yakobo 2:1-7

Ijumaa asubuhi tarehe 27.01.2023

Yakobo 2:1-7

[1]Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu.

[2]Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu;

[3]nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu,

[4]je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu?

[5]Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao?

[6]Bali ninyi mmemvunjia heshima maskini. Je! Matajiri hawawaonei ninyi na kuwavuta mbele ya viti vya hukumu?

[7]Hawalitukani jina lile zuri mliloitwa?

Yesu anaondoa ubaguzi;

Yakobo anaonya juu ya upendeleo katika Kanisa la Mungu. Anatoa mfano wa kumkaribisha vizuri yule aliyevaa vizuri, na kutompokea kwa heshima yule ambaye hajavaa vizuri. Yakobo anayaita hayo "mawazo mabovu". Ukiendelea kusoma unaona Yakobo akisema kuwa upendeleo ni dhambi mbele za Mungu;

Yakobo 2:9

[9]Bali mkiwapendelea watu, mwafanya dhambi na kuhukumiwa na sheria kuwa wakosaji.

Yakobo anaongelea uhalisia ulioko maishani mwetu. Tunabaguana kwa sababu ya tofauti zetu kama fedha, elimu, kabila, rangi n.k kama anavyosema Yakobo, chanzo cha matendo haya ni mawazo mabovu. Tunawaza vibaya ndiyo maana tunatenda vibaya, yaani kubaguana. Tofauti haziwezi kukosa, ila hazitutambulishi kama kundi la waaminio katika ufalme wa Mungu. Tunaalikwa kupendana maana sisi sote ni mwili wa Kristo. 

Siku njema.