Date: 
31-01-2023
Reading: 
Mwanzo 28:16-22

Jumanne asubuhi tarehe 31.01.2023

Mwanzo 28:16-22

[16]Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli BWANA yupo mahali hapa, wala mimi sikujua.

[17]Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni.

[18]Yakobo akaondoka asubuhi na mapema, akalitwaa lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake.

[19]Akaita jina la mahali pale Betheli; lakini jina la mji ule hapo kwanza uliitwa Luzu.

[20]Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae;

[21]nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo BWANA atakuwa Mungu wangu.

[22]Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.

Kung'aa kwa Yesu;

Isaka baada ya kumbariki Yakobo, alimuusia asioe binti za Kanani, bali aende Padan-aram nyumbani kwa babu yake aliyeitwa Bethuel (baba yake Rebeka, mama yake Yakobo) akapate mke huko. Akiwa njiani kuelekea huko aliota ndoto akaona ngazi ambayo malaika walipanda na kushuka, na katika ndoto hiyo Bwana akamuahidi kumpa uzao mkubwa na nchi.

Sasa katika somo la asubuhi hii ndipo tunamuona Yakobo anaamka usingizini na kusema Bwana yuko hapa (pale alipokuwa). Yakobo akasema kuwa Mungu akimfanikisha katika njia aliyokuwa akiiendea, Bwana atakuwa Mungu wake.

Tangu kale Mungu alijidhihirisha kwa watu wake katika mpango wa kuwalinda, kuwaongoza na kuwaokoa watu wake. Alimtokea Yakobo kwenye ndoto, na baadaye kweli alikuwa taifa kubwa. Mungu aliendelea kujifunua kupitia kwa manabii, na baadaye alimtambulisha Yesu kama Mwokozi wa ulimwengu pale alipobatizwa, na hata pale alipong'aa na kubadilika. Kwa kugeuka sura Utukufu wake ulionekana, akiwa tayari kuiendea njia ya mateso. Ni kwa njia ya kifo alituokoa na dhambi na kutupa wokovu. Tudumu katika wokovu huu kwa maisha ya sasa, hata uzima wa milele.

Siku njema.