Date: 
16-01-2023
Reading: 
Mwanzo 14:8-16

Jumatatu asubuhi tarehe 16.01.2023

Mwanzo 14:8-16

8 Mfalme wa Sodoma, na mfalme wa Gomora, na mfalme wa Adma, na mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari, wakatoka wakapanga vita panapo bonde la Sidimu;
9 wapigane na Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu, na Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, wafalme wanne juu ya wale watano.
10 Na bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami. Nao wafalme wa Sodoma na Gomora wakakimbia, wakaanguka huko, nao waliosalia wakakimbia milimani.
11 Wakachukua mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula vyao vyote, wakaenda zao.
12 Wakamtwaa Lutu, mwana wa nduguye Abramu, aliyekaa huko Sodoma, na mali yake, wakaenda zao.
13 Mtu mmoja aliyeponyoka akaenda, akampasha habari Abramu Mwebrania; naye amekaa panapo mialoni ya Mamre, yule Mwamori, ndugu ya Eshkoli, na ndugu ya Aneri, na hao walikuwa wamepatana na Abramu.
14 Abramu aliposikia ya kwamba nduguye ametekwa mateka, akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani.
15 Akajipanga apigane nao usiku, yeye na watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande wa kushoto wa Dameski.
16 Naye akarudisha mali zote, akamrudisha na Lutu nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu.

Nyumba zetu hubarikiwa na Mungu;

Sura ya 13 ya kitabu cha Mwanzo, inaonesha Abramu na Lutu wakiwa na mifugo mingi hadi kugombania malisho (Huyu Abramu ndiye alikuwa  Ibrahimu Mwz 17:5). Abramu akamsihi Lutu, kwamba wao ni ndugu hivyo hawana haja ya kugombana. Wakapatana mmoja aende upande mmoja, mwingine upande mwingine, ili kila mtu achunge mifugo yake kwa furaha.

Sasa somo la asubuhi hii linamuonesha mfalme wa Sodoma na wenzake wakiingia vitani kupigana na himaya za Elamu, Goimu, Shinari, Elasari. Wakifika hadi bonde la Sidimu. Walimtwaa Lutu na na mali zake zote  wakaenda zao! Yaani kwa kifupi Lutu alitekwa, akawa mateka!
Habari hii haikumfurahisha Abramu, akaamua kuwapa vijana wake kazi ya kumkomboa Lutu na mali zake. Alifanikiwa kumkomboa Lutu na kumrejesha akiwa na familia yake, na mali zake.

Tunauona upendo wa Abrahamu kwa Lutu ndugu yake. Hapa lipo somo la kusaidiana kama ndugu katika Kristo.  Tutafakari ni kwa vipi tunasaidiana? Ni kwa kiasi gani wewe ni msaada kwa ndugu yako?
Lakini pia lipo funzo la neema ya Mungu kwa Lutu. Ni kwa neema ya Mungu Lutu aliokolewa toka mateka.  Bwana alimtumia Abramu kumkomboa Lutu. Kumbe Bwana huwa hatuachi katika maisha yetu ya kila siku, hivyo kumfuata kwa uaminifu ni muhimu sana maana yeye ndiye  hubariki nyumba zetu.


Tunakutakia wiki njema