Date: 
24-01-2023
Reading: 
Matendo ya Mitume 11:1-15

Jumanne asubuhi tarehe 24.01.2023

Matendo ya Mitume 11:1-15


[1]Basi mitume na ndugu waliokuwako katika Uyahudi wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu.
[2]Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara wakashindana naye,
[3]wakisema, Uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao.
[4]Petro akaanza kuwaeleza kwa taratibu, akasema,
[5]Nalikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono; chombo kinashuka, kama nguo kubwa inatelemshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikilia.
[6]Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wa nchi wenye miguu minne, na wanyama wa mwituni, nao watambaao, na ndege wa angani.
[7]Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule.
[8]Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijaingia kabisa kinywani mwangu.
[9]Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi.
[10]Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni.
[11]Na tazama, mara hiyo watu watatu wakasimama mbele ya nyumba tuliyokuwamo, waliotumwa kwangu kutoka Kaisaria.
[12]Roho akaniambia nifuatane nao, nisione tashwishi. Ndugu hawa sita nao wakaenda pamoja nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule;
[13]akatueleza jinsi alivyomwona malaika aliyesimama nyumbani mwake na kumwambia, Tuma watu kwenda Yafa ukamwite Simoni aitwaye Petro,
[14]atakayekuambia maneno ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote.
[15]Ikawa nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo.

Yesu anaondoa ubaguzi;

Watu waliokuwa wakiifuata sheria katika Yerusalemu walishindana na Petro wakimwambia kwamba aliingia  kwa watu wasiotahiriwa. Petro akaongea nao taratibu jinsi alivyotokewa na Bwana katika huduma yake hadi kuingia kwa watu walioonekana hawastahili. Lakini Petro alifanya huduma yake hapo wakapokea Roho Mtakatifu. Baada ya mazungumzo ya Petro wale watu wakaamini kwamba huduma ya Yesu ni kwa wote;


Matendo ya Mitume 11:18
[18]Waliposikia maneno haya wakanyamaza, wakamtukuza Mungu, wakisema, Basi, Mungu amewajalia hata mataifa nao toba liletalo uzima.

Hakuna ambaye hastahili kupewa huduma ya neno la Mungu na Sakramenti.
Hakuna asiyehubiriwa. Kwa maana hiyo tunakumbushwa kuitenda kazi ya Bwana kwa watu wote. Tusibague.
Tunapotangaza habari za Yesu Kristo tukumbuke alikuja kwa ajili ya wote, hivyo tuwahubirie. Mbingu ni kwa ajili ya wote waaminio, hivyo ni wajibu wetu kuwafanya wote wamwamini Yesu. 

Siku njema.