Date: 
11-07-2024
Reading: 
2 wathesalonike 3:6-15

Alhamisi asubuhi tarehe 11.07.2024

2 Wathesalonike 3:6-15

6 Ndugu, twawaagiza katika jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni nafsi zenu na kila ndugu aendaye bila utaratibu, wala si kwa kufuata mapokeo mliyoyapokea kwetu.

7 Mwajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu;

8 wala hatukula chakula kwa mtu ye yote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote.

9 Si kwamba hatuna amri, lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate.

10 Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula.

11 Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine.

12 Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe.

13 Lakini ninyi, ndugu, msikate tamaa katika kutenda mema.

14 Na ikiwa mtu awaye yote halishiki neno letu la waraka huu, jihadharini na mtu huyo, wala msizungumze naye, apate kutahayari;

15 lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu.

Bidii ya kijana, mafanikio ya Kanisa;

Wapo watu katika Thesalonike baada ya kupokea Injili walilishika neno la Kristo. Wao ikawa ni kuhubiri tu, ni Kanisani tu, ni kumngoja Bwana. Hawakufanya kazi. Hawa Paulo anawakataa, akielekeza wengine kujitenga na nafsi za watu wa namna hii. Yaani Paulo anazuia njia ya kuamini bila kufanya kazi, akisema kuwa asiyefanya kazi asile. 

Paulo anakataa Injili za kuombaomba. Wapo baadhi yetu wanaosema wameitwa kuhubiri Injili, wao wakiamka asubuhi ni Biblia mkononi wakihubiri mtaani. Hawa sijui huwa wanakula nini? Uwakili wa muda unatuelekeza kufanya kazi sahihi kwa wakati sahihi. Tuache uvivu. Injili ya kweli ni maisha halisi katika Kristo, hivyo tufanye kazi kwa bidii ili kupata mafanikio kwa ajili yetu, lakini muhimu zaidi kwa ajili ya kazi ya Mungu. Amina.

Alhamisi njema.

Heri Buberwa