Date: 
29-06-2024
Reading: 
1 Wafalme 1:49-53

Jumamosi asubuhi tarehe 29.06.2024

1 Wafalme 1:49-53

49 Ndipo wageni wote waliokuwa pamoja na Adonia wakaogopa, wakaondoka, wakaenda zao kila mtu njia yake.

50 Adonia naye akaogopa mbele ya Sulemani; akaondoka, akaenda, akazishika pembe za madhabahu.

51 Akaambiwa Sulemani, kusema, Tazama, Adonia amwogopa mfalme Sulemani; kwani, tazama, amezishika pembe za madhabahu, akisema, Mfalme Sulemani na aniapie leo kwamba hataniua mimi mtumwa wake kwa upanga.

52 Akasema Sulemani, Akionekana kuwa mtu wa kweli, hata unywele mmoja wake hautaanguka chini; lakini uovu ukionekana ndani yake, atakufa.

53 Basi mfalme Sulemani akatuma watu, wakamtelemsha toka madhabahuni. Naye akaja, akamwinamia mfalme Sulemani; naye Sulemani akamwambia, Enenda nyumbani kwako.

Iweni na huruma;

Wakati Daudi akiwa mzee sana, Adonia alijitawaza kuwa mfalme ajaye. Alifanya sherehe kubwa na kuandaa wapanda farasi na walinzi wa kutosha. Ilibidi watu waende kumuuliza mfalme Daudi nani angetawala baada yake maana Adonia alikuwa amejitawaza kuwa mfalme. Daudi hakuchelewa, siku hiyo hiyo akamtawaza Suleimani kuwa mfalme kwa sherehe kubwa zilizofana na kusikika mji mzima.

Ndipo tunaona katika somo Adonia akiogopa, na wote aliokuwa nao wakakimbia. Adonia akamuogopa Suleimani akiomba asimuue kwa upanga. Suleimani akatuma watu wakamleta Adonia, akamwinamia Suleimani, naye Suleimani akamuacha. Suleimani alimuonea huruma Adonia. Nasi tunakumbushwa kuwa na huruma. Amina

Jumamosi njema.

Heri Buberwa