Date: 
21-06-2024
Reading: 
1 Wakorintho 3:18-23

Ijumaa asubuhi tarehe 21.06.2024

1 Wakorintho 3:18-23

18 Mtu asijidanganye mwenyewe; kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima.

19 Maana hekima ya dunia hii ni upuzi mbele za Mungu. Kwa maana imeandikwa, Yeye ndiye awanasaye wenye hekima katika hila yao.

20 Na tena, Bwana anayafahamu mawazo ya wenye hekima ya kwamba ni ya ubatili.

21 Basi, mtu ye yote na asijisifie wanadamu. Kwa maana vyote ni vyenu;

22 kwamba ni Paulo, au Apolo, au Kefa; au dunia, au uzima, au mauti; au vile vilivyopo sasa, au vile vitakavyokuwapo; vyote ni vyenu;

23 nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu.

Umoja wetu, nguvu yetu;

Kanisa la Korintho lilikuwa limegawanyika. Watu walijitenga kimakundi, kila mmoja akiona kundi lake ndilo sahihi. Ukisoma nyuma kidogo ya sura hii ya tatu unaona jinsi walivyogawanyika kulingana na viongozi wao wa kiimani. Hii ilileta mgawanyiko ambao ilibidi Mtume Paulo aukemee.

Angalia Paulo anavyoandika;

1 Wakorintho 3:4-7

4 Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu?
5 Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa.
6 Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu.
7 Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye.

Sasa katika somo la siku, kujiona bora, kujiona na hekima na mengine kama hayo, Paulo anasema ni upumbavu. Anasema watu wa namna hii wapashwa kufundishwa hekima. Kwa maneno mengine watu wa Korintho hawakuwa na umoja. Paulo anasema sisi ni wa Kristo, kwa maana hiyo sisi ni wamoja. Basi tukae katika umoja kama Yesu alivyotuombea, ili kwa umoja wetu tuendelee kutumika pamoja kwa ajili ya Utukufu wake. Amina.

Ijumaa njema.

 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com