Date: 
14-06-2024
Reading: 
2 Timotheo 2:20-26

Ijumaa asubuhi tarehe 14.06.2024

2 Timotheo 2:20-26

20 Basi katika nyumba kubwa havimo vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali na vya mti, na vya udongo; vingine vina heshima, vingine havina.

21 Basi ikiwa mtu amejitakasa kwa kujitenga na hao, atakuwa chombo cha kupata heshima, kilichosafishwa, kimfaacho Bwana, kimetengenezwa kwa kila kazi iliyo njema.

22 Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.

23 Walakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua ya kuwa huzaa magomvi.

24 Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu;

25 akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli;

26 wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.

Heri wenye moyo safi;

Somo la asubuhi ya leo, mstari wa 21 hutumika kuwaambia "waliookoka" kujitenga na wenye dhambi. Kwanza hakuna asiye na dhambi kama neno la Mungu linavyosema;

1 Yohana 1:8-10

8 Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.
9 Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.
10 Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.

Kujitenga kunakosemwa hapa ni maisha tunayoishi kutotutoa kwa Kristo. Yaani tushirikiane na wenzetu, katikati ya changamoto mbalimbali lakini tudumu katika Kristo. Yesu alikula na wenye dhambi, mfano halisi wa upendo. Somo linatufundisha kutokuwa wagomvi, wapole, wavumilivu, tukitenda kwa kadri ya mapenzi yake.

Kama Kanisa la Mungu tunaelekezwa kukaa pamoja tukifundishana na kuhubiriana yapasayo ufalme wa Mungu ili kwa pamoja tuwe na moyo safi, tayari kuurithi uzima wa milele. Mpende jirani yako, huo ndiyo moyo safi.

Ichukie dhambi, mpende mwenye dhambi, maana sisi sote tu wenye dhambi, hivyo tupendane. Amina

Ijumaa njema 

 

Heri Buberwa