Date: 
29-03-2024
Reading: 
Isaya 53:8-9

Hii ni Ijumaa Kuu;

Ijumaa ya tarehe 29.03.2024;

 

Siku ya kukumbuka kifo cha Bwana Yesu;

Masomo;

Zab 22:5-11

1Pet 3:18-22

*Isa 53:8-9

Isaya 53:8-9

8 Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu.

9 Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.

Yesu aliteswa na kufa kwa ajili yetu;

Kitabu cha Isaya sura ya 53, ni utabiri wa mtumishi anayeteseka kwa ajili ya wengine. Isaya anahabarisha wasomaji wake kuwa yupo atakayekuja duniani kuokoa watu, na atateseka kwa ajili yao. Ni utabiri wa ujio wa Yesu Kristo Mwokozi wa ulimwengu, aliyekuja kuteseka kwa ajili ya dhambi za ulimwengu. Ukisoma kuanzia mstari wa 1, unaona jinsi Yesu alivyopitia hali mbalimbali kama kupigwa, kuteswa, kudharauliwa, kuonewa n.k lakini katika yote hayo alikuwa mnyenyekevu. Alijitwika huzuni yetu na masikitiko, akiiendea njia ya msalaba.

Utabiri wa Isaya unaonesha mpango wa Mungu wa wokovu kwa mwanadamu. Hivyo Isaya naye anaujuza ulimwengu, kuwa atakuja Yesu Kristo, ambaye yeye ndiye atakuwa Mwokozi wa ulimwengu, na katika kuokoa atapitia mateso na kifo msalabani.

Hivyo Nabii Isaya tunaweza kusema anatujuza kuwa Yesu Kristo ndiye aliyeteseka na kufa kwa ajili yetu. Ndiye aliyepigwa na kupata kila aina ya mateso, hadi kuwambwa msalabani.

Alidharauliwa;

Wapo waliompokea Yesu, lakini wapo waliomkataa, hadi kumsulibisha. 

Isaya 53:3

[3]Alidharauliwa na kukataliwa na watu; 
Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; 
Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, 
Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu.

Tunapokumbuka kifo chake, tunao wajibu wa kutafakari nafasi yake mioyoni mwetu. 

Tumempokea?

Au tunamdharau?

Tafakari mwenendo wako katika kumfuata Yesu, ili usiwe kama wale waliomdharau na kukataa kumpokea.

Sisi ndiyo sababu;

Kama wazo la siku lilivyo, Yesu aliteswa na kufa kwa ajili yetu. Yaani sisi ndio sababu ya yeye kufa. Dhambi zetu ndio zilimpeleka msalabani. Sasa alikwisha kuzibeba, kwa nini tusitubu na kumgeukia? Baada ya kuteswa, kufa na kufufuka, tulipona, yaani tumeokolewa. Isaya alilisema hili, kuwa baada ya Yesu kufa, wokovu utakuwa tayari;

Isaya 53:5

[5]Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, 
Alichubuliwa kwa maovu yetu; 
Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, 
Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.

Hili ni hakikisho la wokovu.

Kazi au wajibu wetu ni kuchukua hatua ya Imani, tukidumu katika Kristo Yesu maishani mwetu.

Mwaka huu tena tunaadhimisha kumbukumbu ya Yesu kufa msalabani kwa ajili yetu. Unaadhimisha kwa utamaduni tu sababu ya historia? Au kwa tafakuri mahususi kuhusu wokovu?

Tusiadhimishe Ijumaa Kuu kwa sababu ya historia tu, bali historia itusaidie kukumbuka kuwa Yesu alikufa kwa ajili yetu. Hivyo kifo chake kitufanye kutafakari nafasi yetu kwenye maisha ya wokovu, tukiwa na ushuhuda mwema kuelekea uzimani.

Yesu alikufa kwa ajili yetu.

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650

bernardina.nyamichwo@gmail.com