Date:
27-03-2024
Reading:
Zaburi 118:15-16
Juma Takatifu
Jumatano asubuhi tarehe 27.03.2024
Zaburi 118:15-16
15 Sauti ya furaha na wokovu Imo hemani mwao wenye haki; Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
16 Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa; Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
Shangilieni Bwana anakuja;
Zamani kabla ya Kristo, Zaburi ya 118 ilitumika na wana wa Israeli wakati wa kuanza adhimisho la ibada hekaluni wakati wa Pasaka. Lilikuwa ni tangazo la kukiri ukombozi wa Israeli toka Misri, na baadaye uhamishoni. Zaburi iliimbwa kwa kupokezana. Kwa Zaburi hii makuhani na waamini walifanya ibada kumshukuru Mungu kwa ukombozi.
Hata baada ya kufufuka kwa Yesu, Zaburi hii iliendelea kutumika kama sifa kwa Mungu kwa kuwakomboa wanadamu. Yaani ifikapo Pasaka huwa tunaimba Zaburi hii tukimsifu kwa sababu ya kutukomboa kwa njia ya kifo chake. Kwa Zaburi hii huwa tunataja sifa zake.
Mashairi tuliyosoma ni sehemu ya Zaburi hii ya 118, ambapo tunaona sifa kwa Mungu kwamba mkono wake wa kuume hutenda makuu. Hili huwa ni shangilio kwa Yesu mfufuka, ambaye kwa kufufuka kwake tumeokolewa. Wokovu ni tendo kuu kwetu.
Baadhi ya mashairi mengine ambayo tunayatumia sana siku ya Pasaka;
Zaburi 118:22-24
22 Jiwe walilolikataa waashi Limekuwa jiwe kuu la pembeni. 23 Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu. 24 Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia.Hapa huwa tunamkiri Yesu aliye neno kweli toka mbinguni, aliyeshinda kifo na mauti. Yesu alikataliwa, aliteswa, alikufa akazikwa, lakini alifufuka. Wapo waliomuona hafai, lakini alishinda kifo! Hili ndilo jiwe kuu la pembeni, Mwokozi wa Ulimwengu. Tunaishangilia siku ya Pasaka tukishangilia wokovu wetu.
Kama tulivyoona, wana wa Israeli walikuwa wakimsifu Mungu na kumshukuru kwa sababu ya kuwakomboa toka utumwani na uhamishoni. Leo tunapoimba mashairi tuliyosoma, tumsifu na kumshukuru Yesu kwa sababu ya wokovu tukidumu katika yeye ili tuwe na mwisho mwema. Amina.
Heri Buberwa Nteboya
Jumatano
Juma Takatifu 2024