Date: 
26-03-2024
Reading: 
Hagai 2:1-9

Juma Takatifu 

Jumanne asubuhi tarehe 26.03.2024

Hagai 2:1-9

1 Katika mwezi wa saba, siku ya ishirini na moja ya mwezi, neno la Bwana lilikuja kwa kinywa cha Hagai nabii, kusema,

2 Sema sasa na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, na hayo mabaki ya watu, ukisema,

3 Miongoni mwenu amebaki nani aliyeiona nyumba hii katika utukufu wake wa kwanza? Nanyi mnaionaje sasa? Je! Mbele ya macho yenu, siyo kama si kitu?

4 Lakini sasa uwe hodari, Ee Zerubabeli, asema Bwana; nawe uwe hodari, Ee Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, nanyi iweni hodari, enyi watu wote wa nchi hii, asema Bwana; mkafanye kazi, kwa kuwa mimi ni pamoja nanyi, asema Bwana wa majeshi;

5 kama neno lile nililoagana nanyi mlipotoka katika nchi ya Misri; na roho yangu inakaa kati yenu; msiogope.

6 Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, Mara moja tena, ni kitambo kidogo tu, nami nitazitikisa hizo mbingu, na hii nchi, na bahari, na nchi kavu;

7 nami nitatikisa mataifa yote, na vitu vinavyotamaniwa na mataifa yote vitakuja; nami nitaijaza nyumba hii utukufu, asema Bwana wa majeshi.

8 Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa majeshi.

9 Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema Bwana wa majeshi; na katika mahali hapa nitawapa amani, asema Bwana wa majeshi.

Shangilieni Bwana anakuja;

Wayahudi walipotoka uhamishoni wakiongozwa na Zerubabeli mjukuu wa Yeoyakini na kuhani mkuu Yoshua, walikuwa na hamasa kidini na kisiasa. Madhabahu ilijengwa kwa muda mfupi sana na msingi wa hekalu ukawekwa. Hata hivyo walikatishwa tamaa na watu fulani waliopinga ujenzi huo. Kwa muda wa miaka kumi na sita kazi ya ujenzi wa hekalu ilikuwa imesitishwa.

Mungu alimtuma Hagai kutoa ujumbe kwa Wayahudi. Jambo kubwa la ujumbe huo halikuwa kujenga hekalu, bali Mungu kuwa na umuhimu wa kwanza katika maisha yao, na kuwa na uhusiano mwema naye. Wayahudi walitumia visingizio vya waliowapinga, hali mbaya ya uchumi, na ugumu wa maisha kuwa udhuru wa kutotoa umuhimu wa kwanza kwa Mungu na kutoendelea na ujenzi wa hekalu.

Lakini wakati huohuo walijenga nyumba zao na kufanya sherehe mbalimbali. Walitumia gharama kubwa kujenga nyumba zao wenyewe, kwa sababu walijiweka wao mbele kwanza, badala ya Nyumba ya Mungu.

Hagai anaonya kwa kusema kuwa hawana budi kujisahihisha kwa kuacha ubinafsi na unajisi. Uasi na unajisi huleta hukumu bali utii na kujitoa kwa kumtegemea Mungu huwa ni baraka.

Somo tulilosoma linaonesha Bwana akisema kuwa fedha na mali yote ni ya kwake. Anawaita watu kumtumikia akiwaambia kuwa Utukufu wa mwisho utakuwa mkuu kuliko ule wa kwanza. Yaani wakimtumikia Bwana na kumcha watakula mema ya nchi na kustawi kuliko mwanzo.

Watu waliitikia kwa toba. Baada ya majuma matatu walianza kazi ya ujenzi wa hekalu. Hagai alisema kwamba kazi yao inaweka msingi wa Taifa ambalo baadaye litaongozwa na Masihi.

Masihi huyu ndiye Kristo Yesu aliyetuokoa kwa njia ya kifo msalabani. Tuongozwe naye ili tuurithi uzima wa milele. Amina 

 

Heri Buberwa Nteboya 

Juma Takatifu 2024

Jumanne asubuhi