Date: 
29-02-2024
Reading: 
Mwanzo 34:25-31

Hii ni Kwaresma 

Alhamisi asubuhi tarehe 29.02.2024

Mwanzo 34:25-31

25 Ikawa siku ya tatu, walipokuwa wakiumwa sana, wana wawili wa Yakobo, Simeoni na Lawi, nduguze Dina, wakatwaa kila mtu upanga wake, wakaujia mji kwa ujasiri, wakawaua waume wote.

26 Wakawaua Hamori, na Shekemu mwanawe, kwa makali ya upanga, wakamtwaa Dina katika nyumba ya Shekemu, wakatoka.

27 Wana wa Yakobo wakawajilia hao waliouawa, wakauteka nyara mji kwa sababu wamemharibu umbu lao.

28 Wakachukua kondoo zao, na ng'ombe zao, na punda zao, na vitu vilivyokuwamo mjini, navyo vilivyokuwako kondeni.

29 Wakatwaa na mali zao zote, na watoto wao wote, na wake zao, na vyote vilivyokuwamo nyumbani mwao wakavichukua mateka.

30 Yakobo akawaambia Simeoni na Lawi, Mmenitaabisha, kunifanya ninuke vibaya kati ya watu wa nchi hii, Wakanaani na Waperizi; na mimi, kwa kuwa watu wangu ni haba, watanikusanyikia, na kunipiga, nami nitaangamizwa, mimi na nyumba yangu.

31 Nao wakasema, Je! Ni vema amtendee umbu letu kama kahaba?

Mawazo maovu ni chanzo cha ukatili;

Shekemu mwana Amori alimtwaa Dina akalala naye (Dina ni mtoto wa Yakobo aliyemzaa kwa Lea). Amori akatokea mbele ya Yakobo akiomba Dina aolewe na Shekemu. Yakobo na watu wake wakatoa amri ya watu wa Amori na wenzake kutahiriwa. Wakatahiriwa wanaume wote, ili waweze kuwa karibu na jamii ya Yakobo. Sasa akina Amori wakiwa wametahiriwa wanaume wote siku ile ya tatu, ndipo somo linaanzia hapo;

Watoto wa Yakobo bado walikuwa na hasira kwa ndugu yao (Dinah) kulala na Shekemu asiye wa ukoo wao. Wakawavamia akina Amori kwa upanga na kuwaua wanaume wote. Simeoni la Lawi waliongoza kikosi cha mauaji kwa mafanikio makubwa maana walitwaa mali zote, watoto na wake. 

Watoto wa Yakobo walichukia Shekemu alipojitwalia dada yao, wakawaza vibaya na kuua. Walifanya ukatili na kuangamiza watu. Leo kwetu hii ni kinyume na maagizo ya Bwana wetu Yesu Kristo anayetuagiza kutolipiza kisasi, kutokuwa hasira tukiumiza wengine. Tunaagizwa kunena, kuwaza na kutenda vema kwa Utukufu wa Mungu. Tuache ukatili. Amina.

Alhamisi njema 

Heri Buberwa