Date: 
23-08-2023
Reading: 
Mathayo 21:28-32

Jumatano asubuhi tarehe 23.08.2023

Mathayo 21:28-32

[28]Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu.

[29]Akajibu akasema, Naenda, Bwana; asiende.

[30]Akamwendea yule wa pili, akasema vile vile. Naye akajibu akasema, Sitaki; baadaye akatubu, akaenda.

[31]Je! Katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye? Wakamwambia, Ni yule wa pili. Basi Yesu akawaambia, Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu.

[32]Kwa sababu Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini, nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini.

Tuwe wanyenyekevu;

Siku zote nina utata/sikubaliani na baadhi ya walimu na wahubiri ambao hudhani na kwa ujasiri husema kuwa neno la Mungu huhubiriwa ili kuokoa tu. Wanapoongelea neno la Mungu, wanadai linakuwa na ufanisi pale tu, watu wanapookolewa, na lisilo na ufanisi au kushindwa watu wasipoamini.

Nabisha! Kwa uwazi kabisa, neno la Mungu halijawahi kukosa ufanisi wala kushindwa. Mungu anasema hivyo. Neno la Mungu lengo lake ni zaidi ya moja. Ni kwa ajili furaha na wokovu kwao waaminio. Linahubiriwa pia makusudi kwa ajili ya hukumu, aibu na hatia kwao wanaokataa kuamini, wanaolikataa neno, wanaolidharau neno, mara nyingi mhubiri, kwa sababu ya kutokuamini. Katika hali hiyo, neno la Mungu huhubiriwa kuwahukumu wasioamini.

Huu ni ukweli wa kale, unaojulikana, lakini unaopuuzwa na baadhi ya wahubiri. Lengo la wokovu duniani ndio kazi sahihi, lakini lakini maonyo na hukumu inaonekana ni kazi ngeni kabisa ya Injili. Lakini yote ni malengo ya Mungu katika neno lake linapohubiriwa. Ni kazi ya kuonya na kuonyesha hukumu inayoonekana katika somo la leo. Bwana Yesu anaonyesha kuwa viongozi wa wayahudi walikuwa hawaamini, wala hawatubu, wakati wale walioonekana watenda dhambi, yaani watozaushuru na makahaba walitubu na kuamini, wote kwa neno lile lile. Bwana Yesu anaongelea kutokuamini kwao na nguvu ya hukumu.

Bwana Yesu katika somo la leo asubuhi anatoa mfano mfupi, wa watoto wawili waliotumwa kufanya kazi shambani na baba yao. Mmoja alikubali lakini hakwenda. Mwingine alikataa, lakini baadae anajutia kutomtii baba yake, anatubu na kwenda shambani. Bwana Yesu anawauliza, kati ya hao wawili ni nani alitimiza mapenzi ya baba yake? Bila shaka jibu ni yule aliyekwenda shambani, bila kujali alichojibu mwanzo.

Bwana Yesu anawafundisha kuwa, Mungu ni Baba, wayahudi ni mzaliwa wa kwanza aliyeitika wito asifanye, twaweza kusema hakuwa na Imani, yaani wayahudi hawana Imani. Makahaba na watoza ushuru waliokataa neno la Mungu, lakini wakatubu Yohana alipohubiri, hawakutii mwanzo, lakini baadae walitimiza mapenzi ya Baba. Ndipo Bwana Yesu anasema hawa walikuwa wanakwenda mbinguni kabla ya wayahudi.

Hii ni hukumu ya haki kabisa! Ni neno la hukumu! Unafiki uliojaa aibu na kutokuamini kwa wayahudi vinalaaniwa wazi! Wayahudi waliwaona watoza ushuru na makahaba kuwa ni wachafu kuliko wenye dhambi wengine wote, lakini hao wenye dhambi Bwana Yesu aliwaona wenye haki kuliko wayahudi, tena kwa mbali. Imani ya mwenye dhambi anayetubu ni dhahiri na ya mfano kuliko ajionaye mwenye haki pasipo toba na Imani ya kweli.

Leo hii, wengi tuko katika nafasi ya yule kijana wa kwanza aliyesema ndio baba nakwenda shambani. Kuwepo kwetu, Imani tuliyo nayo na toba ni jibu kwa Mungu. Swali; tunaenda kwenye shamba la mizabibu? Au tunasema hivi na kufanya vile? Kama huyu kijana alivyofanya? Wayahudi walitubu bila kuamini. Walifanya mambo ya kidini kwa nje, bila uhalisia wa Imani. Ukweli ni kuwa hawakuliamini neno la Mungu, na hawakumwamini Yesu. Wao waliishi kwa njia zao, na sio Yesu alivyotaka. Hata walipokabiliana na ukweli, hawakufanya toba. Walikasirika, na kutafuta jinsi ya kumnyamazisha mhusika, kama Yohana Mbatizaji na Bwana Yesu. Hawakutaka kukubali kuwa walikosea, ila ukweli walistahili kutubu.

Unanielewa?

Ujumbe huu unakuhusu wewe na mimi. Acha kuwaza kuwa unamhusu fulani. Neno la Mungu halihubiriwi ili umhukumu jirani yako, bali utambue dhambi zako na kutubu. Sheria ya Mungu ni kioo cha kukuonyesha hali yako kiroho. Sio kwa ajili ya kuwaangalia wengine, bali wewe mwenyewe. Baadhi yetu bado hatuamini kinachohubiriwa. Hatutaki kubadilika. Tunahisi kuwa watakatifu kwa kuja Kanisani, kwenda jumuiya na kutoa huduma mbalimbali. Lakini je, tuko kwenye shamba la mizabibu?

Wengi tumekuwa zaidi, au chini ya mtoto aliyesema ndiyo, lakini hakwenda shambani. Sio kwamba mimi sina hatia katika hilo labda kuliko wengine. Ninachojua mimi ni mwenye dhambi. Sijivunii kuwa mwenye dhambi! Lakini naukubali kama ukweli, kwa sababu muda mwingi naandaa mahubiri, na ninaona yananihusu! Mimi mwenye dhambi! Nahitaji kutubu. Wewe je?

Tunapotubu dhambi zetu zinasamehewa. Bwana Yesu alilipa yote msalabani. Mungu hakukusubiri wewe, wala mimi, aliuchukua udhaifu wetu nakutusafisha dhambi zetu kwa njia ya kifo cha Bwana Yesu msalabani. Tunapoujua ukweli huu na kuamini kuwa Mungu hutupenda, tunakuwa katika nafasi ya kuurithi uzima wa milele.

Tunapotubu pia, tunakuwa kama yule kijana aliyejibu hapana, katika dhambi, baadaye alijuta na kwenda shambani. Kazi yetu kubwa katika shamba la mizabibu ni kuamini. Tunapoliamini neno la Mungu, tunatubu, maana neno la Mungu litatupa unyenyekevu kutambua dhambi na hitaji letu. Neema ya Mungu inatuita kujutia dhambi zetu, na kudumu shambani mwa Bwana tukitenda yatupasayo kwa utukufu wake.

Swali ambalo asubuhi hii nakuuliza?

Uko kwenye shamba la mizabibu?

Tunapofakari kuwepo kwetu kwenye shamba la mizabibu, tuendelee kujiuliza maswali yafuatayo;

1. Unatimiza mapenzi ya Baba?

Bwana Yesu baada ya kueleza kuhusu hao watoto wawili, anauliza, “ni yupi alitimiza mapenzi ya baba yake”? Bila shaka hapa ni yule aliyekwenda shambani. Hapa wayahudi walikuwa wanaambiwa kuwa kutimiza mapenzi ya Baba ni muhimu. Yaani ni hivi; kutimiza mapenzi ya Baba yetu wa mbinguni ni muhimu sana. Yule baba alitaka watoto waende shambani. Baba yetu anatuita kutenda mema. Tafakari mambo (dhambi) yanayokuzuia kutenda mapenzi ya Baba leo na kuchukua hatua. Kama umekubali kwenda shambani, hudumia mizabibu. Kama umekubali kumfuata Bwana Yesu, fanya mapenzi yake. Unatimiza mapenzi ya Baba?

 2. Uko kama Wayahudi au watoza ushuru na makahaba?

Tumeona awali, kuwa wayahudi walipokea Injili lakini hawakuamini, wala hawakumpokea Bwana Yesu! Makahaba na watoza ushuru hawakupokea Injili, lakini walipohubiriwa walimpokea Bwana Yesu. Wewe uko kama nani?

3. Maamuzi yako kwa sasa ni yapi?

Katika somo la leo, aliyeamua kwa usahihi ni yule aliyeamua kwenda shambani. Alishaamua vingine hapo mwanzo. Tunaweza kuwa tumeshaamua mambo mengi ambayo yametuzuia kwenda shambani. Mungu anatuita kufanya maamuzi sahihi, yaani kurejea na kukaa kwake. Fanya uamuzi wa kutubu na kuamini, na uendelee kuishi kwa msaada wa Mungu mwenyewe.

Unaamua nini?

Asubuhi hii itika sauti ya Bwana, inayokuita kwenda shambani na kutenda kadri ya mapenzi yake. 

Dumu shambani, hudumia mizabibu. Kaa kwa Yesu, ukitimiza mapenzi yake. Kuwa mnyenyekevu.

Jumatano njema

 

Heri Buberwa