Jumanne asubuhi tarehe 22.08.2023
Danieli 5:25-31
25 Na maandiko yaliyoandikwa ni haya; MENE, MENE, TEKELI, NA PERESI.
26 Na tafsiri ya maneno haya ni hii; MENE, Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha.
27 TEKELI, umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka.
28 PERESI, ufalme wako umegawanyika, nao wamepewa Wamedi na Waajemi.
29 Ndipo Belshaza akatoa amri, nao wakamvika Danielii mavazi ya rangi ya zambarau, wakatia mkufu wa dhahabu shingoni mwake, wakapiga mbiu kutangaza habari zake, ya kwamba yeye ni mtu wa tatu katika ufalme.
30 Usiku uo huo Belshaza, mfalme wa Wakaldayo, akauawa.
31 Na Dario, Mmedi, akaupokea ufalme, naye umri wake alikuwa na miaka sitini na miwili.
Tuwe wanyenyekevu;
Mfalme Belshaza alifanya karamu kubwa kabisa, akawaalika watu wengi kula karamu. Aliagiza viletwe vyombo vitakatifu toka hekaluni, akaamuru vitumike katika karamu hiyo! Basi vyombo vikatolewa, karamu ikaendelea. Mara kikatokea kiganja cha mkono kikiandika ukutani.
Mfalme alifadhaika sana, akaita waganga, wapiga ramli, wachawi na wanajimu ili watafsiri maneno yaliyoandikwa. Wote walishindwa. Mke wa mfalme akamwendea mfalme akimtambulisha Danieli, ambaye alikubali kutafsiri ndoto bila gharama yoyote.
Danieli alimwambia Mfalme Belshaza habari za ukuu wa Mungu tangu enzi za Baba yake Mfalme Nebuchadreza hadi alivyoondolewa kitini kwa sababu ya kutompa Mungu Utukufu. Danieli akamwambia Belshaza naye kuwa amekosa kuwa mnyenyekevu kwa kutumia vyombo vitakatifu vya hekaluni;
Danieli 5:22
Na wewe, mwanawe, Ee Belshaza, hukujinyenyekeza moyo wako, ijapokuwa ulijua hayo yote.Danieli alimwambia Mfalme kwamba kwa kutumia vyombo vitakatifu, Mfalme alikosa unyenyekevu. Sasa ndipo maandishi yale yakaletwa mbele ya Danieli, yaliyoandikwa MENE, MENE, TEKELI na PERESI, ambayo tafsiri yake ilimaanisha kuwa ufalme wake mfalme Belshaza ulikuwa umefikia mwisho. Mfalme Belshaza alikufa usiku huo huo. Kukosa unyenyekevu kulimuondoa mamlakani na alikufa. Kukosa unyenyekevu kunatuondoa kwa Kristo. Tuwe wanyenyekevu ili tusiondoke kwa Kristo. Amina.
Jumanne njema.
Heri Buberwa