Date: 
21-08-2023
Reading: 
Mika 6:6-8

Jumatatu asubuhi tarehe 21.08.2023

Mika 6:6-8

6 Nimkaribie Bwana na kitu gani, na kuinama mbele za Mungu aliye juu? Je! Nimkaribie na sadaka za kuteketezwa, na ndama za umri wa mwaka mmoja?

7 Je! Bwana atapendezwa na elfu za kondoo waume, au na elfu kumi za mito ya mafuta? Je! Nimtoe mzaliwa wangu wa kwanza kwa kosa langu, mzao wa mwili wangu kwa dhambi ya roho yangu?

8 Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!

Tuwe wanyenyekevu;

Wakati wa Nabii Mika, Wayahudi hawakuwa wema kwa maskini. Walitumia sheria kwa manufaa yao wenyewe. Waliwakopesha fedha wahitaji kwa riba kubwa, na pale wahitaji waliposhindwa kulipa kwa wakati walinyang'anywa mali zao, hadi nguo zao! Soma hapa;

Mika 2:8-9

8 Lakini siku hizi mmeinuka kama adui za watu wangu; mwaipokonya joho iliyo juu ya nguo za hao wapitao salama kama watu wasiopenda vita.
9 Wanawake wa watu wangu mwawatupa nje ya nyumba zao nzuri; watoto wao wachanga mwawanyang'anya utukufu wangu milele.

Lakini katika sura ya 6, Nabii Mika analeta ujumbe kuwa Mungu ni mwenye haki. Mungu ndiye aliyewapandisha Israeli kwenye nchi ya ahadi kutokea utumwani Misri. Katikati ya maisha ndani ya nchi ya ahadi, ndipo matendo ya kupora haki za wengine yanaendelea. Matajiri walipora haki za wengine lakini wakiendelea kumwabudu Mungu na kutoa sadaka. Yaani Mungu aliwatendea haki, lakini wao hawakutenda haki.

Pamoja na wao kutoa sadaka hekaluni, Mika anakazia katika mstari wa 8 kwamba Mungu ni wa haki kama tulivyousoma hapo juu. Usome tena;

Mika 6:8

Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako!

Somo linatukumbusha kufanya yote kwa utukufu wa Mungu, lakini kubwa zaidi kumwendea Mungu kwa unyenyekevu. Amina.

Uwe na wiki njema yenye unyenyekevu.

 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com