Date: 
09-08-2023
Reading: 
Mathayo 10:5-15

Jumatano asubuhi tarehe 09.08.2023

Mathayo 10:5-15

5 Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie.

6 Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.

7 Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.

8 Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.

9 Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu;

10 wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake.

11 Na mji wo wote au kijiji cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hata mtakapotoka.

12 Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni.

13 Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi.

14 Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni mwenu.

15 Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule.

Tuenende kwa hekima;

Yesu Kristo anawatuma wanafunzi wake kuhubiri Injili. Anawatuma kutoa huduma ya uponyaji, kufundisha na kuwarejesha watu kwake. Katika kazi hiyo anawatuma na kuwahakikishia kuwa wapo watu watakaowapokea na kuwatunza. Watakapowapokea, wahubiri ufalme wa Mungu, na pale watakapowakataa wakung'ute mavumbi miguuni na kuondoka.

Yesu anapowaambia wanafunzi wake jinsi ya kuingia kwenye nyumba za watu, kwamba waingie na kuhubiri na pengine wakikataliwa wakung'ute mavumbi na kuondoka, anawaambia kutumia hekima, maana ilibidi kutambua nyumba hizo. Kwa njia hiyo hiyo, nasi tunaelekezwa kuifanya kazi ya Mungu kwa hekima itokayo kwake ili kuzaa matunda. Amina.

Siku njema.

Heri Buberwa