Date: 
19-07-2023
Reading: 
1Yohana 3:10-12

Jumatano asubuhi tarehe 19.07.2023

1 Yohana 3:10-12

10 Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.

11 Maana, hii ndiyo habari mliyoisikia tangu mwanzo, kwamba tupendane sisi kwa sisi;

12 si kama Kaini alivyokuwa wa yule mwovu, akamwua ndugu yake. Naye alimwua kwa sababu gani? Kwa sababu matendo yake yalikuwa mabaya, na ya ndugu yake yalikuwa ya haki.

Amri ya Upendo;

Yohana anaandika kwamba watoto wa Mungu hudhihirika, wa Ibilisi nao. Watoto wa Mungu hutenda haki, lakini wa shetani hutenda uovu. Yohana anaitaja haki mojawapo kuwa ni upendo, kwamba yeyote asiye na upendo ni wa shetani. Yohana pia anarejea historia kuwa Kaini alimuua Abeli kwa sababu matendo yake (Kaini) hayakuwa ya haki.

Upo mkazo kwamba asiye na upendo ni mwuaji;

1 Yohana 3:15-16

15 Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake.
16 Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu.

Basi na tupendane kama lilivyo agizo la Kristo, tusiwe wauaji. Pendo la Kristo litawale katikati yetu. Amina.

Siku njema.

 

Heri Buberwa