Jumamosi asubuhi tarehe 04.02.2023
Isaya 42:1-9
[1]Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu.
[2]Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu.
[3]Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli.
[4]Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake.
[5]Mungu BWANA anena, yeye aliyeziumba mbingu, na kuzitanda; yeye aliyeitandaza nchi na mazao yake; yeye awapaye pumzi watu walio juu yake; yeye awapaye roho wao waendao ndani yake.
[6]Mimi, BWANA, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa;
[7]kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa.
[8]Mimi ni BWANA; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu.
[9]Tazama, mambo ya kwanza yamekuwa, nami nayahubiri mambo mapya; kabla hayajatokea nawapasheni habari zake.
Kung'aa kwa Yesu Kristo;
Nabii Isaya alikuwa akitabiri juu ya Mtumishi mteule wa Mungu, Yesu Kristo ambaye Baba alimtoa kuleta wokovu kwa wanadamu. Alimtambulisha kama mwenye nguvu, ambaye kazi yake isingezuiliwa na yoyote. Akijitambulisha kama mtumishi mteule, Yesu anarejea unabii huu wa Isaya katika Injili ya Mathayo;
Anarejea kama ifuatavyo;
Mathayo 12:18-21
[18] Tazama, mtumishi wangu niliyemteua;
Mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye;
Nitatia roho yangu juu yake,
Naye atawatangazia Mataifa hukumu.
[19]Hatateta wala hatapaza sauti yake;
Wala mtu hatasikia sauti yake njiani.
[20]Mwanzi uliopondeka hatauvunja,
Wala utambi utokao moshi hatauzima,
Hata ailetapo hukumu ikashinda.
[21]Na jina lake Mataifa watalitumainia.
Yesu alirejea unabii huu wa Isaya baada ya kumponya mtu mwenye mkono uliopooza (Mt 12:9-14). Alikuwa akionesha nguvu na mamlaka yake, maana Mafarisayo walitafuta kumshtaki baada ya kumponya aliyepooza mkono siku ya sabato. Utabiri huu wa Isaya ni tangazo la Yesu Mwokozi aliyeng'aa na kudhihirika kama mwanakondoo aichukuaye dhambi ya ulimwengu. Tunaalikwa kudumu katika Kristo aliyedhihirika kwetu, ili tupate neema yake katika kazi zetu, na hatimaye uzima wa milele.
Jumamosi njema.
Heri Buberwa