Jumatano asubuhi tarehe 01.02.2023
2 Wakorintho 3:4-11
[4]Na tumaini hilo tunalo mbele za Mungu kwa njia ya Kristo.
[5]Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lo lote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu.
[6]Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha.
[7]Basi, ikiwa huduma ya mauti, iliyoandikwa na kuchorwa katika mawe, ilikuja katika utukufu, hata Waisraeli hawakuweza kuukazia macho uso wa Musa, kwa sababu ya utukufu wa uso wake; nao ni utukufu uliokuwa ukibatilika;
[8]je! Huduma ya roho haitazidi kuwa katika utukufu?
[9]Kwa maana ikiwa huduma ya adhabu ina utukufu, siuze huduma ya haki ina utukufu unaozidi.
[10]Maana hata ile iliyotukuzwa haikuwa na utukufu hivi, kwa sababu ya utukufu uzidio sana.
[11]Kwa maana, ikiwa ile inayobatilika ilikuwa na utukufu, zaidi sana ile ikaayo ina utukufu.
Kung'aa kwa Yesu;
Ni ujumbe wa Mtume Paulo kwa Kanisa la Korintho, kwamba wao ni wahudumu wa Agano jipya. Paulo anaonesha kuwa waliweza kutenda kazi kwa njia ya Kristo, ambaye ndiye aliwatosheleza. Anakumbusha kuwa Israeli walipokea amri kupitia kwa Musa, lakini kutoka kwa Mungu, kwa Utukufu wa Mungu. Anawahimiza watu wa Korintho kudumu katika utume kwa kuitegemea nguvu ya Kristo Yesu.
Ujumbe wa Mtume Paulo leo asubuhi ni kuwa utume wetu ni lazima uwe kwa Kristo, tukimtegemea Kristo mwenyewe. Tofauti na hapo ni ubatili. Yesu alipong'aa sauti ilitoka mbinguni;
Luka 9:35
[35]Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye.
Ndiyo maana leo asubuhi Paulo anatukumbusha kumsikia na kumtegemea Yesu katika utume wetu. Katika utume wako unamtegemea nani?
Uwe na Jumatano njema
Heri Buberwa