Date: 
09-09-2025
Reading: 
1 Wafalme 13:20-22

Jumanne asubuhi tarehe 09.09.2025

1 Wafalme 13:20-22

20 Hata ikawa, walipokuwa wameketi mezani, neno la Bwana likamjia nabii yule aliyemrudisha;

21 akamlilia yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda, akinena, Bwana asema hivi, Kwa sababu umeiasi kauli ya Bwana, wala hukuishika amri ile aliyokuamuru Bwana, Mungu wako,

22 bali umerudi, ukala chakula ukanywa maji, hapo alipokuambia, Usile chakula, wala usinywe maji; maiti yako haitaliingia kaburi la baba zako.

Tutumie ndimi zetu kwa Utukufu wa Mungu;

Yupo mjumbe wa Mungu toka Yuda alipeleka ujumbe wa toba katika Betheli. Hakupokelewa vizuri, maana hata Mfalme alimnyooshea mkono ili wamkamate, mkono wake Mfalme ukakatika! Mfalme akamlilia yule mjumbe wa Mungu, mkono ukarudishwa. Yule mjumbe wa Mungu akashika njia kurudi alikotoka, kwa njia nyingine kama alivyokuwa ameambiwa na Bwana. Mfalme Yeroboamu akamuomba aende naye nyumbani kwake angalau apate chakula, yule mjumbe wa Mungu akakataa kwamba Bwana alimzuia.

Pale Betheli kulikuwa na nabii mwingine mzee, akasikia habari za mjumbe huyu wa Mungu na kilichotokea hekaluni Betheli. Akamfuata yule mjumbe wa Mungu arudi kula nyumbani kwake. Fahamu kwamba huyu mjumbe alikuwa ameambiwa asile chochote na kunywa katika Betheli. Lakini huyu nabii mzee alimshawishi, akarudi akala nyumbani kwake. Baada ya kula akaondoka, akavamiwa na Simba akauawa! (Soma kuanzia mstari wa 1)

Tunachoona hapa ni kwamba yule mjumbe wa Mungu aliyetumwa katika Betheli alizuiwa kula huko, lakini alishawishiwa na nabii mzee katika Betheli akakubali. Alishawishiwa kwa ulimi, na kwa ulimi wake akakubali, matokeo yake akauawa na Simba! Tuwe makini na matumizi ya ulimi, maana matokeo ya maneno yake yaweza kuwa hasi kwetu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla. Vishawishi vinakuja kwa njia ya maneno yanayosemwa na ulimi, sikiliza na uamue kwa busara. Amina

Jumanne njema

Heri Buberwa Nteboya 

Mlutheri 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com