Event Date: 
13-07-2025

Siku ya Jumapili tarehe 13 Julai 2025 ilikuwa ni Siku ya Vijana katika Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral, siku ambayo huadhimishwa kila mwaka ili kutambua na kuthamini mchango wa vijana katika kulijenga na kuliendeleza neno la Bwana.

Katika siku hiyo muhimu kwa vijana na usharika kwa ujumla, vijana wa Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral walipata fursa ya kuongoza ibada zote tatu za siku hiyo. Akitoa mahubiri ya siku hiyo kwa ibada za Kiswahili, Bi Hellen Lutahakana, aliwaasa vijana kuwa chachu ya kuleta maendeleo katika jamii zao bila kuacha imani zao kwa Mungu. 

“Vijana tumekuwa na mambo mengi yanayotusumbua katika jamii ikiwa ni pamoja na kutamani mafanikio ya haraka na kuwa na tamaa za kimwili. Tumwombe Mungu atusaidie katika mchakato wa kufikia maendeleo tunayoyatamani,” alisema Hellen.

Katika hatuaa nyingine, Hellen alisema kutokana na ukuaji wa teknlojia ya mawasiliano kumekuwa na njia nyingi za kupata taarifa na maarifa hususani kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii. Hellen aliwasisitiza vijana kutumia mitandao hiyo kwa lengo la kujifunza mambo yanayompendeza Mungu na kwa ajili ya kujiletea maendeleo. 

“Tunamshukuru Mungu kwamba pamoja na uwepo wa changamoto nyingi katika teknlojia ya mitandao, lakini pia kuna faida, maana tunaweza kujifunza neno la Mungu kupitia hiyo hiyo teknolojia,” alisema.

Kwa upande wa ibada ya Kiingereza mhubiri alikuwa Victoria Silkiluwasha ambaye pia alitoa msisitizo juu ya vijana kufanya kazi kwa bidii huku wakimtegemea Mungu.

Neno na mafundisho katika siku ya vijana mwaka 2025 yalitoka katika kitabu cha 2 Wafalme 22: 1-2 yakibebwa na kichwa cha neno kisemacho Kijana Mkristo Ni Chachu Ya Maendeleo”  

Baadhi ya picha kutoka kwenye ibada za siku hiyo.