Hii ni Epifania;
Jumatatu ya tarehe 06.01.2025
Siku ya Ufunuo;
Masomo;
Zab 112:1-4
2Kor 4:6
*Mt 4:12-16
Mathayo 4:12-16
12 Basi Yesu aliposikia ya kwamba Yohana amefungwa, alikwenda zake mpaka Galilaya;
13 akatoka Nazareti, akaja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali;
14 ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema,
15 Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, Njia ya bahari, ng'ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa,
16 Watu wale waliokaa katika giza Wameona mwanga mkuu, Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti Mwanga umewazukia.
Yesu ni nuru ya Ulimwengu;
Epifania ni nini?
Neno Epifania linatokana na neno la Kiyunani "epiphaneia" likimaana "udhihirisho". Ni siku ambayo wakristo huadhimisha udhihirisho wa kwanza wa Yesu kwa mataifa. Udhihirisho huu huwasilishwa na wale wataalamu wa nyota (Mt 2:1-12) walivyoifuata ile nyota ya Mashariki hadi kumuona. Pia udhihirisho huo wa kiimani ni kama ulivyotokea Yesu akibatizwa mtoni Yordani na ishara yake ya kwanza kule Kana ya Galilaya. Epifania ni mojawapo ya sikukuu tatu za zamani sana katika Kanisa, nyingine zikiwa ni Noeli na Pasaka. Kanisa Katoliki la Rumi, Makanisa mengi ya Kilutheri, Anglikana na mengine baadhi huadhimisha sikukuu hii siku ya tarehe 06 mwezi wa kwanza (kama leo), siku 12mbaada ya Noeli, wakati baadhi ya makanisa ya Mashariki ya Orthodox huadhimisha siku hii tarehe 19.01 maana wao huadhimisha Noeli tarehe 06.01. Maelezo yafuatayo yanasimulia kwa ufupi;
i) Sikukuu ya Epifania huadhimishwa tarehe 06.01 ikiwa ni alama ya kumaliza mzunguko wa "nuru" katika kalenda ya Liturjia ya Kanisa. Mzunguko huu huanza na Majilio, huendelea na Noeli, na humalizika na Epifania ambayo humaanisha udhihirisho au Ufunuo. Siku ya adhimisho huwa haibadiliki maana hufuata kalenda ya kawaida.
ii) Katika adhimisho hili, mambo matatu hukumbukwa katika Epifania ambayo ni wataalamu wa nyota kwenda kumuona Yesu (Mt 2:1-12), Ubatizo wa Yesu kwenye mto Yordani (Mt 3:1-12, Luka 3:21-22, Mk 1:1-9) na ishara ya maji kuwa divai huko Kana (Yn 2:1-11)
iii) Umuhimu wa Epifania kiTheologia ni pale Yesu alipofunuliwa kama Mwana wa Mungu, aliyefanyila mwanadamu. Yaani neno aliyefanyika mwili kwa ajili ya ukombozi wa wanadamu. Mtume Paulo anatumia maudhui ya Epifania kueleza Yesu alivyofunuliwa kwetu na ujio wake kwa mara ya pili;
2 Timotheo 1:9-10
[9]ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele, [10]na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili;Tito 2:13
[13]tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu;2 Wathesalonike 2:8
[8]Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake;iv) Adhimisho la kale kabisa lilifanyika huko Alexandria, Misri katika karne ya tatu. Inaaminika kuwa lilikuwa ni adhimisho la hujuma, ambapo Kanisa lililenga kukabiliana na sherehe za ''aion" mungu wa wakati ule katika Misri, sherehe ambazo zilichukuliwa kama ni za kubadilisha maji kuwa divai (Andrew Dragos, 2018)
v) Ni Injili ya Mathayo tu ambayo inawataja Mamajusi ambao wanatajwa kama wataalamu wa nyota toka Mashariki (tafsiri baadhi huwataja kama werevu, na nyingine wafalme) soma Dan 1:20; 2:2; uone majukumu yao katika mabaraza. Idadi yao haitajwi lakini hudhaniwa kuwa walikuwa wengi. Kwamba walikuwa watatu, hiyo hutajwa kwa sababu walitoa zawadi tatu, yaani uvumba, tunu na manemane kuashiria mwanadamu aliye Mungu kweli na mfalme. Maana yake Yesu alidhihirika kwao.
vi) Mamajusi walikwenda kumuona mtoto Yesu nyumbani na siyo horini kama wale Wachungaji tuliowasoma siku ya Noeli. Hii ilitokea miaka miwili baada ya Yesu kuzaliwa. Asili ya Mamajusi haijulikani, japokuwa huonekana kuwa walitokea Peresi au Babiloni. Baadhi ya wasomi wa Agano la kale husema kuwa Mamajusi walijifunza na kupata habari za kuja kwa Mesiya kutoka kwa Wayahudi (kama anavyoandika Nabii Danieli) na waliyafahamu maandiko ya zamani (Agano la kale) ingawa hitimisho la hili siyo halisi (the evidence for this is inconclusive). Lengo hapa ni kuona Yesu alivyodhihirika kwa ulimwengu, haikuwa rahisi.
vii) Nyota zilifahamika kuwa na ishara mbaya kwa watawala. Hivyo Mfalme Herode, myahudi asiye mwaminifu kwa viwango vya wakati ule alihisi dalili mbaya kwa utawala wake. Maandiko hayaelezi nyota iliashiria nini, hoja hapa ni kuwa nyota ilikuwa njia ya Yesu kudhuhirika.
Nimeandika kwa kirefu kidogo ili upate mwanga kuhusu sikukuu hii ya Epifania, Siku ambayo tunaadhimisha jinsi Yesu alivyodhihirika kwa ulimwengu.
Sasa tukirudi kwenye somo la Epifania leo;
(Soma tena somo la mahubiri juu mwanzoni tena)
Huduma ya Yesu inaanza baada ya kujaribiwa kwake, na habari za kufungwa kwa Yohana. Ingawa sura ya 12 inasema Yesu alikwenda Galilaya, safari hii ilikuwa ya hatari. Kama Mathayo anavyoeleza, mtawala wa Galilaya, Herode (Antipas) ndiye aliyekuwa amemfunga Yohana. Kumfunga Yohana ilionekana kama huduma ya Yesu kufunikwa! Kapernaumu ambao kulikuwa nyumbani kwa Yesu, ulikuwa mji wa watu takribani 1000. Wakazi wake walikuwa wakulima na wavuvi. Ingawa Yesu alikuwa amekwisha kutajwa kama mwana wa Mungu, hakuishi kati ya wenye nguvu na matajiri, bali kati ya watu wa kawaida. Kapernaumu ilikuwa Kaskazini Magharibi mwa ufukwe wa bahari ya Galilaya
Mkoa huu kwa historia ulikuwa kwa ajili ya makabila ya Zabuloni na Naftali, lakini katika karne ya kwanza lilikuwa eneo la "Galilaya ya mataifa" (soma Mathayo 4:15 akinukuu Isaya 9:1), chini ya utawala wa Rumi. Herode (Antipas) alikuwa kiongozi mwenye sifa mbaya na katili ambaye alikuwa tayari kumuangamiza yeyote aliyekuwa kinyume na utawala wake. Katikati ya hatari hii na kifo, Yesu anatangaza ukombozi, kuwa yeye ni nuru ya Ulimwengu (16).
Ujumbe wa Yesu ni kama ule wa Yohana, "Tubuni maana ufalme wa mbinguni umekaribia". Ujumbe huu wa toba unasomeka toka Mathayo 3:2 Yohana akiutoa, halafu sasa Yesu mwenyewe anautoa kwenye Mathayo 4:17. Pamoja na kuwa maudhui ni yaleyale, mazingira ni tofauti. Yohana alikuwa mtangulizi aliyeandaa njia, na Yesu akawa ukamilifu wa ujumbe. Katika ujumbe huo, ndipo Yesu anakuja na habari nuru kuangazia Ulimwengu. Kama Yohana, Yesu anawaita watu kutubu. Kitenzi cha Kiyunani "kutubu" (metanoeo), kama Kitenzi cha Kihebrania "kutubu" (shub) maana yake ni kugeuka (turn around). Kutubu kiTheologia siyo tu kuomba msamaha, bali kubadilika, kubadili uelekeo, tabia, maisha n.k Hiki ndicho Yesu anahubiri, toba.
Yesu ni nuru ya Ulimwengu;
Katika somo la leo, Yesu anaposema waliokaa katika nchi ya uvuli na mauti mwanga umewazukia anaonesha unabii wa yeye kuja kutimia. Anamnukuu Isaya;
Isaya 9:2
Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza.
Kwa hiyo nuru hii ni Yesu mwenyewe anayewaambia watu kutubu, yaani wageuke na kuacha njia mbaya. Tukiwa bila Yesu tunakuwa gizani. Yesu aliye nuru anatuangazia pale tunapompokea na kumpa maisha yetu. Tutubu dhambi zetu, tugeuke na kumcha yeye daima ili tuurithi uzima wa milele. Amina
Heri Buberwa Nteboya
Epifania 2025