Event Date: 
29-09-2024

Siku ya Jumapili tarehe 29 Septemba 2024 katika Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front ilifanyika Sikukuu ya Mikaeli na Watoto; Sikukuu ambayo hufanyika kila mwaka kwa ajili ya kumkumbuka malaika Mikeli na watakatifu wote pamoja na watoto. Ibada hii hufanyika kwa kuongozwa na watoto wakisaidiana na walimu wao pamoja na watumishi wengine wa usharika (parish workers).

Kwa mwaka wa 2024, Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front zilifanyika ibada tatu kuadhimisha sikukuu hiyo, ibada za Kiswahili mbili na moja ya Kiingereza. Katika ibada zote tatu watoto walipata fursa ya kuongoza shughuli zote za ibada ikiwemo kusoma litrugia, matangazo pamoja na kuongoza sala. Somo; Mithali 22: 6; Tuwajali Watoto Na Mikaeli.

Akihubiri katika ibada zote tatu za siku hiyo, Mwalimu Ephraim Sanga, aliwaasa washarika, wazazi pamoja na walezi kuhakikisha wanawalea watoto katika njia zinazompendeza Mungu nyakati zote. “Huwezi kumlea mtoto vizuri kama wewe mwenyewe (mzazi) umeshindwa kujilea vizuri”, alisema. Mwalimu Ephraim pia aliwaasa wazazi na walezi kuwajengea watoto utamaduni wa uwajibikaji, kumwamini Mungu, kuwa watiifu na kufanya kazi kwa bidii.

Wazazi tuendelee kumwomba Mungu atupe busara ili ikimpendeza yeye (Mungu), watoto wetu pia waweze kurithi busara zetu na hata wao waweze kurithisha kizazi kijacho,” Mwalimu Ephraim aliongeza. 

Pia katika ibada zote tatu watoto walipata fursa ya kusema mistari ya moyo, kufanya ngonjera na kuimba nyimbo mbalimbali. Vyote hivyo vilibeba ujumbe kwa wazazi kuhusu kuwalea watoto vyema ili wakue katika maadili mema ya kikristo.

Kwa upande wake, Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front, Chaplain Charles Mzinga, aliwaasa wazazi na walezi kuacha utamaduni wa kuwapa watoto wao simu janja ili wachezee kwani wanaweza kuona vitu visivyofaa. Pia, Chaplain Mzinga aliwaasa wazazi na walezi kuwapa watoto wao muda wa kutosha wa kupumzika na kufuatilia kwa karibu maendeleo yao shuleni na hata kanisani. “Watoto wanajifunza kwa kuiga kutoka kwetu, basi tuwe wazazi/ walezi wazuri,” aliongeza.

Mapema siku ya Jumamosi tarehe 28 Septemba 2024, watoto walikusanyika katika viwanja vya Usharika ambapo walipata fursa ya kushiriki katika shughuli mbalimbali ikiwemo kuonyesha vipaji vyao; kuchora, kuimba, kucheza pamoja na kukata keki.

Angalia picha zaidi hapa chini;

Matukio mbalimbali katika picha wakati wa ibada za Mikaeli na Watoto zilizofanyika katika Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front, tarehe 29-30/09/2024. Picha: AZF Media Team.

 

Angalia ibada zote hapa:

Ibada ya KWANZA - Kiswahili: https://www.youtube.com/watch?v=JF5N2K114XE&t=5963s

Ibada ya PILI - English: https://www.youtube.com/watch?v=RfAvIu04ZF4&t=3150s

Ibada ya TATU - Kiswahili: https://www.youtube.com/watch?v=mtQ7cl-LUbE

---------- MWISHO -----------