Jumanne asubuhi tarehe 01.10.2024
Mathayo 18:1-6
[1]Saa ile wanafunzi wakamwendea Yesu wakisema,
[2]Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao,
[3]akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.
[4]Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.
[5]Na ye yote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi;
[6]bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari.
Tuwajali watoto wetu katika Bwana;
Injili ya Mathayo imegawanyika katika sehemu tano kama ifuatavyo;
i) Sehemu ya 1 ni sura ya 5 hadi 7 ambayo huitwa mahubiri ya mlimani, na yamenukuliwa sehemu nyingi katika Agano jipya. Sehemu hii inazo "Heri" na Sala ya Bwana. Kwa wamwaminio Yesu, mahubiri/hotuba ya mlimani hutoa maelekezo ya uanafunzi.
ii) Sehemu ya pili (sura ya 10) hutoa maelekezo kwa wanafunzi wa Yesu, na wakati mwingine huitwa "maelezo ya utume"
iii) Sehemu ya tatu (13:1-53) hutoa mifano kuhusu ufalme wa Mungu. Sehemu hii huitwa maelezo ya mifano
iv) Sehemu ya nne (sura ya 18) huitwa maelezo juu ya Kanisa. Huusisha mifano kama kondoo aliyepotea, mtumwa asiyesamehe, yote kuhusu ufalme wa Mungu. Maudhui makubwa hapa huhusu mwisho wa waaminio.
v) Sehemu ya tano (23,24 na 25) huitwa maelezo kwenye mlima wa mizeituni. Pia huitwa sehemu ya maelezo ya nyakati za mwisho, maana huongelea pia hukumu ya mwisho. Kuna maudhui ya ujio wa Yesu mara ya pili.
Sasa basi;
Somo la leo ni mwanzo wa sehemu ya nne ya injili ya Mathayo, inayohusu maisha ya pamoja katika Kanisa. Nachukulia kwamba ni habari kuhusu maisha ya Kanisa kwa sababu nafikiri wanafunzi waliuliza maswali kama vile;
-Nani mkuu katika ufalme wa Mungu?
-Nani kiongozi wetu?
-Nani kiongozi wetu?
-Nani mfuasi wa kweli?
-Unampenda nani zaidi?
-Nani muumini wa kweli?
-Nani ana mawazo sahihi?
-Nani kati yetu ni muhimu zaidi?
-Nani mkuu?
Kumbuka hapa waliuliza hivi, lakini Yesu alikuwa amekwishakuwafundisha jinsi ya kuenenda, ili kuuona ufalme wa Mungu, nyuma kwenye Heri (5:1-12)
Ni kwamba walikuwa hawakumbuki?
Hawakuelewa?
Walitaka kuelewa zaidi?
Walitaka fundisho jingine, labda lile la Heri waliona haliwafai?
Yesu alikuwa na njia nyingi za kujibu, lakini alichagua njia ya mtoto mdogo. Alipomweka mtoto kati yao hawakuelewa. Yesu akaanza kuueleza ufalme wa mbinguni akimtumia mtoto mdogo! Kwamba yeyote anyenyekeaye kama mtoto mdogo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa Mungu. Watoto wadogo huwa hawana hatia. Kwa maneno mengine anatutaka kuishi maisha ya kutokuwa na hatia. Ni magumu sana! Bila neema haiwezekani!
Kwa upande mwingine naweza kusema kuwa kama Yesu hamaanishi kuwa watoto hawana hatia, basi anatuhitaji kuwa wanafunzi wazuri kama watoto, tukijifunza yatupasayo kuhusu ufalme wa Mungu. Yesu aapotuita kuwa wanafunzi wazuri, kwa mfano wa watoto, ni wazi anatuita kumtegemea yeye kama watoto wawategemeavyo wazazi kwa kila kitu.
Binadamu hutegemea wazazi wao sio kwa dakika, bali miaka. Kuuingia ufalme wa Mungu kama mtoto ni kuangalia utegemezi wetu kwa Mungu na kujifunza kumuamini na kumtegemea kwa kiwango asichoweza kufikia mwanadamu. Hivyo kuuingia katika ufalme wa Mungu kama mtoto maana yake ni sisi kuwa wanafunzi wazuri, kutambua utegemezi wetu kwa Mungu na uvumilivu.
Watoto huamini wazazi
Watoto hupokea
Watoto huomba wazazi wao
Watoto hufundishika kwa urahisi....na mengine mengi
Kwa maana hiyo, mtoto bila mzazi au mlezi maisha yake huwa hatarini. Na hapo Yesu ndipo anatufundisha leo kuwa sisi bila yeye maisha yetu yako hatarini.
Haiwezekani Yesu alikuja fundisho hili bila sababu. Nimeeleza hapo awali juu y wanafunzi kutaka kujua zaidi, lakini pia kuna hoja ya wazi kuwa inawezekana hali ya kujishusha miongoni mwa wanafunzi ilikuwa ina walakini. Inaweza kuwa sababu pia ya Yesu kutumia mfano wa mtoto, kujibu swali lao.
Kumbe ni wakati tujichunguze, kama kweli tunanyenyekea kama watoto mbele ya Mungu katika kuuendea ufalme wake. Bila kuwa kama mtoto ni vigumu kuuona ufalme wa Mungu.
Nitumie mfano halisi wa Suleimani; aliyeomba kwa unyenyekevu neema ya Mungu kuelekea utume alioitiwa;
1 Wafalme 3:7
[7]Na sasa, Ee BWANA, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia.Mungu alimfanya mkubwa katika utume wake. Kumbe nasi tukinyenyekea kama watoto wadogo, Mungu hutufanya wakubwa katika ufalme wake.
Tuwajali watoto wetu katika Bwana;
Pamoja na kuelekezwa kuwa watiifu na wanyenyekevu kama watoto, tunaelekezwa pia kuwapenda na kuwajali watoto ili wadumu katika utii wao, katika ufalme wa Mungu;
Tunawapendaje?
Tunawajali vipi?
1. Kwa kuwapa neno la Mungu;
Hili halina mjadala. Watoto lazima tuwawekee msingi imara katika Kristo Yesu. Tuwapeleke ibadani, tusali nao nyumbani mwetu, tukisoma nao neno la Mungu. Tuliagizwa toka zamani;
Kumbukumbu la Torati 6:4-7
[4]Sikiza, Ee Israeli; BWANA, Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja. [5]Nawe mpende BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. [6]Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; [7]nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.Mtume Paulo pia ameandika;
Waefeso 6:4
[4]Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana.
Maonyo ya Bwana anayoyasema Mtume Paulo ni neno la Mungu. Kanisa halijaweka siku hii kwa bahati mbaya. Ni kutukumbusha kuwa tunahitaji kuwaleta watoto kwa Bwana Yesu, na bila kufanya hivyo Kanisa lijalo halitakuwa imara. Sisi tumefika hapa kwa sababu tuliandaliwa na wazazi wetu. Tunapowapa watoto neno la Mungu tunaliandaa Kanisa la kesho. Nini nafasi yako katika hili?
2. Tuwape elimu.
Tunawajibika kuwapa elimu watoto wetu ili waweze kuyamudu mazingira yao, lakini waweze kumtolea Mungu. Hapo tunajenga Kanisa linalojitegemea. Kanisa lazima liweze kuhubiri lenyewe Injili, lionekane linakua, liweze kujitegemea (Mchg. Prof. Wilson Niwagila). Sasa hatuwezi kujenga Kanisa la namna hii bila kuwekeza kwa watoto. Njia mojawapo ya kufanya hivi ni kuwapa watoto wetu elimu. Hatuwezi kuwapa watoto wetu elimu bora kama hatuwapendi na kuwajali.
3. Tuwatie moyo.
Njia mojawapo ya kuwapenda watoto wetu ni kuwawezesha katika wanayoyafanya tukiwatia moyo. Hii inaweza kuwa katika vipaji na kazi zao. Hapa tunaweza kujenga vipaji ambavyo pia ni muhimu katika kuendesha maisha yao kama kuimba, kucheza mpira n.k
4. Tuwafundishe kufanya kazi;
Maisha ya Magharibi yametuteka kiasi kwamba kwa sasa ni jambo la kawaida mtoto kuhitimu darasa la 7, wakati mwingine kidato cha nne akiwa hajui kufua shati lake! Yaani hawezi hata kusonga ugali wake tu! Huu ndiyo utandawazi? (Prof. Chachage Seth Chachage aliita utandawizi)
Huu utandawazi usiofundisha watoto wetu kuwajibika ni upuuzi! Haiwezekani kujenga jamii ya watu wasiojua kufanya kazi! Hapa tutakuwa tunadumisha tamaduni za kishenzi. Fundisha mtoto wako kupika, kulima, usafi na kazi nyinginezo ili asiwe mzigo baadae kwa mwenzake na jamii kwa ujumla, labda kama una mpango wa kukaa naye milele hapo nyumbani kwako.
Mwisho;
Yesu anatuita kuwa watiifu na wanyenyekevu kama watoto wadogo. Pamoja na kuwa kama watoto, tunaitwa kuwatunza watoto ili wadumu katika ufalme wa Mungu. Tukiwatunza watoto ipasavyo, watazidi kuwa mfano bora kwetu, kuuelekea ufalme wa Mungu. Amina
Tuwajali watoto wetu katika Bwana;
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650