Date: 
17-09-2024
Reading: 
Wakolosai 2:16-17

Jumanne asubuhi tarehe 17.09.2024

Wakolosai 2:16-17

16 Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato;

17 mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.

Uhuru wetu katika Kristo Yesu;

Mtume Paulo anawaambia Wathesalonike kwamba mtu asiwahukumu kwa vyakula au vinywaji, sikukuu, mwandamo wa mwezi, sabato n.k Anawataka kuishi kwa kutoyaangalia hayo maana ni mambo ya sheria. Ni maisha waliyoishi kwa kuifuata torati ya Musa, ambapo walijiona kuwa wakamilifu kwa kuifuata hiyo torati. Yaani mtu alionekana mkamilifu kwa kuifuata torati!

Ujumbe tunaopewa ni kumfuata Kristo aliye mkamilifu na utimilifu wa torati. Kristo ndiye alikuja kuitimiliza torati kama alivyosema;

Mathayo 5:17

Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.

Wapo ambao husema kwa mstari huu katika hotuba ya mlimani, Yesu aliisimika torati rasmi. Tena wanakazia kwa mstari unaofuatia;

Mathayo 5:18

Kwa maana, amin, nawaambia ,Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka ,hata yote yatimie.

-Yesu alichomaanisha ni kuwa yeye alikuja kuitimiliza torati. Tunaposema torati haina nafasi bali Kristo, ni kuwa torati isomwe kwa mtazamo wa Kristo aliye utimilifu wa torati na Mwokozi wa ulimwengu. 

Tusihukumiwe kwa aina za maisha kwa sababu tu ni torati imesema, bali kwa kuisoma torati tumwangalie Kristo aliye utimilifu wa vyote. Vyakula, vinywaji, sabato, mwezi mwandamo n.k havina nafasi kwetu kuliko Uhuru tulio nao katika Kristo Yesu. Mwamini sasa uokolewe. Amina

Jumanne njem

Heri Buberwa