Date: 
13-09-2024
Reading: 
Kumbukumbu la Torati 12:10-14

Ijumaa asubuhi 13.09.2024

Kumbukumbu la Torati 12:10-14

10 Lakini mtakapovuka Yordani na kukaa katika nchi anayowarithisha Bwana, Mungu wenu, akawapeni raha, akiwaokoa na adui zenu pande zote, mkakaa salama;

11 wakati huo itakuwa kwamba mahali pale atakapopachagua Bwana, Mungu wenu, alikalishe jina lake, hapo ndipo mtakapoleta kila kitu ninachowaamuru; sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu zote teule mtakazoweka kwa Bwana.

12 Nanyi mtafurahi mbele za Bwana, Mungu wenu, ninyi, na wana wenu, na binti zenu, na watumishi wenu wanawaume na wanawake, na Mlawi aliyemo malangoni mwenu; kwa kuwa hana sehemu wala urithi kwenu.

13 Ujihadhari usitoe sadaka zako za kuteketezwa katika kila mahali upaonapo;

14 bali katika mahali atakapopachagua Bwana katika kabila zako mojawapo, ndipo utakapotoa sadaka zako za kuteketezwa, ndipo utakapotenda yote nikuamuruyo.

Uwakili wetu kwa Mungu;

Jana asubuhi tuliona maelekezo ya Mungu kwa watu wake kutoa sadaka kwake, na siyo kwa miungu mingine. Maelekezo yalikuwa ni kutoa sadaka hekaluni mwa Bwana. Somo la leo ni mwendelezo wa lile la jana, ambapo Israeli wanapewa ahadi ya kukombolewa kutoka utumwani, na baada ya kukombolewa wanaagizwa kumtolea Mungu sadaka. 

Tunakumbushwa kumtolea Mungu shukrani zetu, tukimshukuru kwa neema yake ya wokovu. Hatuwezi kuulipia wokovu, wala hakuna kiasi tunachoweza kutoa kulipia wokovu, bali tunatoa sehemu ya mali alizotupa kumshukuru na kwa ajili kazi yake. Tukumbuke tulivyookolewa, tumtolee Mungu shukrani zetu. Amina

Ijumaa njema

Heri Buberwa