Date: 
31-07-2024
Reading: 
Marko 1:40-45

Jumatano asubuhi tarehe 31.07.2024

Marko 1:40-45

40 Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa.

41 Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika.

42 Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika.

43 Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara,

44 akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao.

45 Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi, na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini kwa wazi; bali alikuwako nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila mahali.

Mungu hupendezwa na mwenye moyo wa toba;

Ndugu mwenye ukoma alimfuata Yesu akiomba utakaso na Yesu akamhurumia akamtakasa, yaani akamponya. Ukoma ulimtoka ule ndugu akawa mzima. Pamoja na Yesu kumzuia kusema popote, yeye alienda siyo kusema tu, bali kuhubiri akisimulia jinsi Yesu alivyomponya. Bila shaka alijawa imani, na furaha sana.

Msingi wa somo letu kwa tafakari ya juma hili ni mstari wa 40 (kuwa na moyo wa toba) ambapo tunaona mwenye ukoma akimpigia Yesu magoti na kuomba kuponywa ukoma. Bila shaka Yesu alipendezwa naye, akamponya. Ndivyo Yesu anavyopendezwa nasi tunapotubu dhambi zetu, hutuhurumia na kutupa msamaha wa dhambi. Tubu dhambi zako, Yesu anakungoja. Amina

Jumatano njema

 

Heri Buberwa 

Mlutheri