Date: 
03-06-2024
Reading: 
Malaki 3:13-16

Jumatatu asubuhi tarehe 03.06.2024

Malaki 3:13-16

13 Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno juu yako kwa namna gani?

14 Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za Bwana wa majeshi?

15 Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao.

16 Ndipo wale waliomcha Bwana waliposemezana wao kwa wao. Naye Bwana akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao waliomcha Bwana, na kulitafakari jina lake.

Chagueni mtakayemtumikia;

Sura ya tatu ya Malaki inaanza na ujumbe unaotabiri ujio wa Kristo ambao umenukuliwa na Injili zote zinazofanana. Ujumbe huo unasema hivi;

Malaki 3:1

Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi.

Ujumbe huu ulilenga kuwaambia watu habari ya ukombozi ambao ungeletwa na Yesu Kristo. Baada ya mstari huo wa kwanza, ujumbe unakuwa watu kukaa katika Bwana kwa kutenda mema wakimngoja Kristo. Ndiyo maana katika somo tunasoma Malaki akiwaambia watu kuwa maneno yao yamekuwa magumu sana kwa Bwana. Yaani waliacha kumtumikia Bwana, maana waliona hakuna faida. 

Ukisoma zaidi unaona kuwa mstari wa 17 ni wito wa kumtumikia Bwana, ambapo Malaki anasema wamtumikiao Bwana watakuwa wake;

Malaki 3:17

Nao watakuwa wangu, asema Bwana wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; naam, watakuwa hazina yangu hasa; nami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye.

Tunaalikwa kumtumikia Bwana daima. Amina.

Tunakutakia wiki njema yenye ushuhuda na mafanikio.

 

Heri Buberwa Nteboya 

Mlutheri 

0784 968650