Hii ni Advent
Jumamosi asubuhi tarehe 23.12.2023
Luka 1:57-66
57 Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume.
58 Wakasikia jirani zake na jamaa zake ya kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye.
59 Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria.
60 Mamaye akajibu akasema La, sivyo; bali, ataitwa Yohana.
61 Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo.
62 Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita.
63 Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohana. Wakastaajabu wote.
64 Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu.
65 Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya milima milima ya Uyahudi.
66 Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye.
Itengenezeni njia ya Bwana;
Injili ya Luka inasimulia kuzaliwa kwa Yohana kulivyokuwa, na Yesu pia. Tangu kuzaliwa, Yohana anaonekana kumtangulia Yesu kwa miezi sita. Hii inadhihirika Malaika anapomtokea Mariamu;
Luka 1:34-37
34 Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? 35 Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. 36 Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; 37 kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.Somo la asubuhi hii ni juu ya kuzaliwa kwa Yohana. Tunasoma jinsi alivyozaliwa hadi kuitwa Yohana kama Bwana alivyoagiza. Mstari wa 66 unaonesha kuwa mkono wa Bwana ulikuwa pamoja na Yohana.
Kinachoonekana ni Yohana kumtangulia Yesu, maana kuzaliwa kwa Yesu kunakuja baada ya kuzaliwa kwa Yohana. Lakini zaidi ya hapo, ni jinsi Yohana aliye mtangulizi wa Yesu alivyoandaliwa toka Zakaria akifukiza uvumba hekaluni hadi kuwa Yohana Mbatizaji.
Yohana huyu ndiye alikuja kuleta ujumbe wa Yesu Kristo, akiwaita watu kuandaa mioyo yao kumpokea. Ujumbe huo hudumu daima, ukitutaka kuwa na mioyo safi wakati wote ili Kristo akae kwetu siku zote. Amina.
Siku njema.
Heri Buberwa