Date: 
07-12-2023
Reading: 
Isaya 11:11-16

Hii ni Advent 

Alhamisi asubuhi tarehe 07.12.2023

Isaya 11:11-16

11 Na itakuwa katika siku hiyo, Bwana atapeleka mkono wake mara ya pili, ili ajipatie watu wake watakaosalia, kutoka Ashuru, na kutoka Misri, na kutoka Pathrosi, na kutoka Kushi, na kutoka Elamu, na kutoka Shinari, na kutoka Hamathi, na kutoka visiwa vya bahari.

12 Naye atawatwekea mataifa bendera, atawakutanisha watu wa Israeli waliotupwa, atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika, kutoka ncha nne za dunia.

13 Na wivu wa Efraimu utaondoka, na wale wanaomwudhi Yuda watakatiliwa mbali; Efraimu hatamhusudu Yuda, wala Yuda hatamwudhi Efraimu.

14 Nao watashuka, watalirukia bega la Wafilisti upande wa magharibi; nao pamoja watawateka wana wa mashariki; watanyosha mkono juu ya Edomu na Moabu; na wana wa Amoni watawatii.

15 Na Bwana atauangamiza kabisa ulimi wa bahari ya Misri; na kwa upepo wake uteketezao atatikisa mkono wake juu ya Mto, naye ataupiga, uwe vijito saba, na kuwavusha watu wenye viatu vikavu.

16 Itakuwako njia kuu kwa mabaki ya watu wake watakaobaki, watokao Ashuru, kama vile ilivyokuwako kwa Israeli, katika siku ile waliyotoka katika nchi ya Misri.

Bwana analijia Kanisa lake;

Isaya anaianza sura ya 11 kwa kutabiri ujio wa Kristo Yesu. Anasema Mfalme atazaliwa kutokea kwenye uzao wa Yese;

Isaya 11:1-2

1 Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.
2 Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana;

Sasa katika mstari wa 11 anasema Bwana kwa njia ya shina la Yese atajitwalia watu waliosalia. Yaani watu wake wataokolewa kwa njia ya Yesu Kristo. Huyu Yesu anatajwa kukutanisha watu waliotawanyika kutoka pande zote za dunia. Hapa ni muhimu kukumbuka kuwa ujumbe huu ulikuja kabla ya Israeli kwenda uhamishoni. Hivyo ahadi ya Mungu inakuja kuwaambia kukombolewa na Bwana, ambaye hakuishia kuwatoa uhamishoni, bali kumtuma Yesu kuwakomboa.

Ahadi hii ya Mungu kuokoa ulimwengu huishi hata sasa. Kwamba Yesu Kristo ndiye Bwana na Mwokozi wetu daima. Huyu ndiye tumwabuduye, ambaye kwa utukufu atakuja kuwahukumu walio hai na wafu. Jiandae kumpokea. Amina.

Alhamisi njema.

Heri Buberwa