Jumatatu asubuhi tarehe 31.07.2023
Yona 4:5-11
5 Ndipo Yona akatoka mjini, akaketi upande wa mashariki wa mji, akajifanyia kibanda huko, akakaa chini yake uvulini, hata aone mji ule utakuwaje.
6 Na Bwana Mungu aliweka tayari mtango, akaufanya ukue juu ya Yona, ili uwe kivuli juu ya kichwa chake, na kumponya katika hali yake mbaya. Basi Yona akafurahi sana kwa sababu ya ule mtango.
7 Lakini siku ya pili kulipopambazuka, Mungu akaweka tayari buu, nalo likautafuna ule mtango, ukakatika.
8 Basi ikawa, jua lilipopanda juu, Mungu akaweka tayari upepo wa mashariki, wenye hari nyingi; jua likampiga Yona kichwani, hata akazimia, naye akajitakia kufa, akasema, Ni afadhali nife mimi kuliko kuishi.
9 Mungu akamwambia Yona, Je! Unatenda vema kukasirika kwa ajili ya mtango? Naye akasema, Ndiyo, natenda vema kukasirika hata kufa.
10 Bwana akamwambia, Wewe umeuhurumia mtango, ambao hukuufanyia kazi, wala kuuotesha; uliomea katika usiku mmoja, na kuangamia katika usiku mmoja;
11 na mimi, je! Haikunipasa kuuhurumia Ninawi, mji ule mkubwa; ambao ndani yake wamo watu zaidi ya mia na ishirini elfu, wasioweza kupambanua katika mkono wao wa kulia na mkono wao wa kushoto; tena wamo wanyama wa kufugwa wengi sana?
Wema wa Mungu watuvuta tupate kutubu;
Yona alitumwa na Mungu kwenda kuhubiri Ninawi,lakini alikataa akapanda meli kwenda Tarshishi. Upepo mkali uliipiga ile meli hadi kukaribia kuvunjika. Abiria waliamua kupiga kura ikamwangukia Yona, akatupwa baharini maana ilionekana ndiye alikuwa chanzo cha meli kupata dhoruba.
Mungu alituma samaki kummeza Yona, ambapo akiwa kwenye tumbo la samaki aliomba rehema. Samaki akamtapika Yona pwani. Yona ilibidi aendelee na wito alioitiwa huko Ninawi. Ujumbe wa Mungu kupitia kwa Yona ulihusu watu wa Ninawi kumgeukia Mungu, ujumbe ambao watu wote waliupokea wakavaa magunia kutoka kwa mkubwa hadi kwa aliye mdogo.
Mungu aliwarehemu watu wa Ninawi;
Yona 3:10
Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.Lakini jambo la ajabu, Yona hakufurahishwa na watu wa Ninawi kumrudia Mungu!
Yona 4:1-2
1 Lakini jambo hili lilimchukiza Yona sana, naye akakasirika. 2 Akamwomba Bwana, akasema, Nakuomba, Ee Bwana; sivyo hivyo nilivyosema, hapo nilipokuwa katika nchi yangu? Hii ndiyo sababu nalifanya haraka kukimbilia Tarshishi; kwa maana nalijua ya kuwa wewe u Mungu mwenye neema, umejaa huruma, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, nawe waghairi mabaya.Yona anapeleka ujumbe wa Mungu lakini anakasirika kwa sababu ya watu kumrudia Mungu!
Hakutaka watubu? Alitaka waangamie? Hakujua kwamba hiyo siyo tabia ya Mungu.
Tunaona mambo mawili;
1. Yona alikataa kwenda Ninawi, lakini Mungu alimrehemu.
2. Watu wa Ninawi pamoja na kumuasi Bwana, aliwarehemu.
Mungu alimtuma Yona kwa wema wake ili watu wa Ninawi watubu. Kwa wema huo anatuita nasi kutubu dhambi zetu na kumuishia yeye siku zote. Amina.
Tunakutakia wiki njema yenye ushuhuda na mafanikio.
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650