Event Date: 
14-04-2023

Hivi karibuni Kwaya ya Agape inayohudumu katika ibada ya Kiswahili kila Jumapili saa moja asubuhi katika Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral iliwatembelea watoto wenye mahitaji mbalimbali katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kuwapa mkono wa faraja.

Watoto walionufaika na ziara hiyo ni wale wenye matatizo ya ugonjwa wa mgongo wazi na wale wenye matatizo ya vichwa vikubwa. Ziara ya kuwatembelea watoto hao ilifanyika tarehe 14/4/2023 ambapo mbali na kupatiwa mahitaji ya siku hadi siku watoto hao pia walipata bima za afya (watoto 100).

Akizungumza wakati wa kukabidhi mahitaji hayo, Katibu Msaidizi wa Kwaya ya Agape Ndg Maiko Nkya alisema kwaya hiyo imejiwekea utaratibu wa kutoa sadaka ya kuwatembelea watoto hao angalau mara moja kwa mwaka ambapo mpaka sasa watoto zaidi ya 450 wamekwisha nufaika kwa kupatiwa kadi za bima ya afya ambazo zinawawezesha kupata matibabu bila malipo katika hospitali na vituo vya afya mbalimblai nchini Tanzania. “Hawa ni watoto wanaohitaji huduma za matibabu kwa muda mrefu na bahati mbaya wengi hawajiwezi kugharamia hizo huduma hivyo sisi kama kwaya tukaona tujikite zaidi katika kuwapatia kadi za bima ya afya,” alisema Nkya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tiba – MOI Dkt. Samuel Swai aliishukuru Kwaya ya Agape kwa kuendelea kujitoa kusaidia jamii kwa kuwafikia watu wenye uhitaji hususani watoto wadogo wenye changamoto mbalimbali za kiafya. Kadhalika, Dkt Swai alitumia fursa hiyo kuishauri jamii kuzingatia matumizi ya vyakula vyenye folic acid hasa kwa akina mama wajawazito ili kupunguza uwezekano wa watoto kuzaliwa wakiwa na matatizo ya vichwa vikubwa.

Kitu muhimu sana katika kupambana na ugonjwa huu ni kuwagundua waathirika mapema ili kuwasaidia haraka iwezekanvyo. Mtoto mwenye matatizo haya akigundulika mapema anatibiwa na kuwa mtoto wa kawaida kabisa,” alisema Dkt Swai.

Kwaya ya Agape inatoa shukrani kwa washarika wote wa Azania Front Cathedral kwa kuchangia fedha na vitu mbalimbali vilivyofanikisha zoezi hilo lililoleta tabasamu katika nyuso za watoto. Mungu awabariki.

*************************************

Picha kutoka MOI - Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Mkurugenzi wa Tiba – MOI Dkt. Samuel Swai akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanakwaya wa Kwaya ya Agape mara baada ya Kwaya hiyo kukabidhi vitu na mahitaji mbalimbali kwa watoto hospitalini hapo.