Date: 
06-03-2023
Reading: 
Matendo ya Mitume 21:27-36

Hii ni Kwaresma

Jumatatu asubuhi tarehe 06.02.2023

Matendo ya Mitume 21:27-36

27 Basi zile siku saba zilipokuwa karibu kutimia, Wayahudi waliotoka Asia wakamwona ndani ya hekalu, wakawataharakisha watu wote, wakamkamata,

28 wakapiga kelele, na kusema, Enyi wanaume wa Israeli, tusaidieni. Huyu ndiye mtu yule afundishaye watu wote kila mahali kinyume cha taifa letu na torati na mahali hapa. Tena, zaidi ya haya, amewaingiza Wayunani katika hekalu, akapatia unajisi mahali hapa patakatifu.

29 Kwa maana walikuwa wamemwona Trofimo, Mwefeso, pamoja naye mjini, ambaye walidhania ya kuwa Paulo amemwingiza katika hekalu.

30 Mji wote ukataharuki, watu wakakutanika mbio mbio, wakamkamata Paulo, wakamkokota, wakamtoa hekaluni; mara milango ikafungwa.

31 Na walipokuwa wakitafuta njia ya kumwua, habari zikamfikilia jemadari wa kikosi ya kwamba Yerusalemu imechafuka, mji mzima.

32 Mara akatwaa askari na maakida, akawashukia mbio. Nao walipomwona jemadari na askari wakaacha kumpiga Paulo.

33 Kisha jemadari akakaribia, akamshika, akaamuru afungwe kwa minyororo miwili; akauliza, Nani huyu? Tena, amefanya nini?

34 Wengine katika makutano wakapiga kelele wakisema hivi, na wengine hivi. Basi alipokuwa hawezi kupata hakika ya habari kwa sababu ya zile kelele, akatoa amri aletwe ndani ya ngome.

35 Basi Paulo alipofika darajani ilikuwa kuchukuliwa na askari kwa sababu ya nguvu ya makutano.

36 Maana kundi kubwa la watu wakamfuata, wakipiga kelele, na kusema, Mwondoe huyu.

Ukatili ni uovu;

Paulo Yuko Yerusalemu (31) akihubiri habari njema za Yesu Kristo. Baadhi ya Wayahudi hawakuwa hawakumwamini, na wala hawakuwa tayari kumsikiliza. Walimkamata na kumpiga, na zaidi ya hapo walitaka kumuua! Mkuu wa askari ndiye aliamrisha wamuache. Ukiendelea kusoma sura ya 22, unaona Paulo akipewa nafasi ya kuhutubia.

Paulo alihutubia akitoa historia ya yeye kukutana na Yesu, jinsi alivyoingia katika utume, akiwaalika waliomsikiliza kumwamini Yesu. Lakini bado walikuwa na roho ngumu;

Matendo ya Mitume 22:22-24

22 Wakamsikiliza mpaka neno lile, wakapaza sauti zao, wakisema, Mwondoe huyu katika nchi, kwa maana haifai aishi.
23 Walipokuwa wakipiga kelele na kutupa mavazi yao na kurusha-rusha mavumbi juu,
24 yule jemadari akaamuru aletwe ndani ya ngome, akisema aulizwe habari zake kwa kupigwa mijeledi, ili ajue sababu hata wakampigia kelele namna hii.

Paulo anaonekana kufanya kazi katikati ya watu wenye mioyo migumu. 

Walikuwa na ukatili hadi kwa watumishi wa Mungu akiwemo Paulo mwenyewe! Yaani walimpiga na kumweka kizuizini Mtume wa Bwana!

Huwezi kupambana na kazi ya Mungu! Ukipambana na Injili utashinda kwa muda na kuangamia milele. Ila ukisimamia Injili utapoteza kwa muda, lakini utafanikiwa milele kama Mtume Paulo.

Mungu atuwezeshe kuisimamia kweli ya neno lake, pia tuache ukatili maana ni uovu.

Nakutakia wiki njema yenye kupinga ukatili.

 

Heri Buberwa