Hii ni Epifania
Jumatatu asubuhi tarehe 09.01.2023
Matendo ya Mitume 2:37-42
[37]Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
[38]Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.
[39]Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.
[40]Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi.
[41]Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu.
[42]Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali.
Ubatizo wetu;
Ilikuwa ni siku ya Pentekoste aliposhuka Roho Mtakatifu, Mitume wakaanza kunena kwa lugha. Baadhi ya waliokuwepo wakadhani Mitume wamelewa kwa mvivyo. Petro ndipo akasimama na kuhutubia mkutano akihubiri habari za Yesu Kristo aliyekufa na kufufuka, na sasa aliyewahushia Roho Mtakatifu. Anatoa historia tangu zama za kale Yesu alivyotabiriwa, alivyokuja, kazi alizofanya hadi kufa na kufufuka, pia walivyomkataa. Waliposikia hotuba yake wakauliza; tufanye nini basi? Tutendeje ndugu zetu?
Ndipo katika somo la leo asubuhi tunasoma Petro akiwaambia kutubu dhambi na kubatizwa ili wapate ondoleo la dhambi. Mstari wa 38 ni msingi wa somo la asubuhi hii;
Matendo ya Mitume 2:38
[38]Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.Siku ile tu walibatizwa watu elfu tatu, wakawa wakidumu kwenye fundisho la mitume na ushirika wa Kikristo.
Asubuhi ya leo tunakumbushwa kuwa kwa njia ya ubatizo tumempokea Yesu Kristo. Wajibu wetu ni kudumu katika mafundisho sahihi ya neno la Mungu, kama watoto wa Mungu. Kwa kubatizwa tumeokolewa, hivyo tunawajibika kudumu katika wokovu kwa kumtegemea Yesu tu. Ubatizo umetuleta kwa Yesu, hivyo tubaki kwa Yesu.
Tafakari kama njia zako ni sahihi mbele za Mungu, kwa ubatizo wako.
Uwe na wiki njema yenye ushuhuda