Date: 
06-06-2022
Reading: 
Marko 3:28-29

Jumatatu ya Pentekoste; Tarehe 06.06.2022.

Masomo;
Zab 106:1-5
1Kor 14:1-5
*Mk 3:28-29

Marko 3:28-29
28 Amin, nawaambia, Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote;
29 bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele,

Kuenea kwa Roho Mtakatifu;

Sura ya tatu ya Injili ya Marko inaonesha jinsi watu tofauti walivyoyachukulia mafundisho na mamlaka yake. Mafarisayo walifikia kupanga njama za kwenda kinyume naye. Makundi ya waliomfuata na kumsikiliza yalianza kuwa tishio kwa mamlaka. Familia yake Yesu waliogopa na kwa usalama wakawa wakitaka kumficha Yesu. Lakini wafuasi wa kweli walionekana. Wale kumi na wawili waliungana na kuwa kitu kimoja, wakati huo kundi lingine lililovutiwa na mafundisho ya Yesu zaidi ya ishara lilipata heshima ya kuwa  familia ya Yesu.

Marko 3:34  Akawatazama wale walioketi wakimzunguka pande zote, akasema, Tazama, mama yangu na ndugu zangu!

Somo lenyewe;
Uķianzia nyuma kidogo, Mafarisayo toka Galilaya walitaka kumwangamiza;

Marko 3:6  Mara wakatoka wale Mafarisayo, wakawa wakifanya shauri juu yake pamoja na Maherodi, jinsi ya kumwangamiza.


Waandishi walianza kumtuhumu kwamba alitenda ishara kwa nguvu ya pepo. Imani yao hii ilimfanya Yesu awatuhumu kufanya kufuru na kuwaonya kuwa wasingesamehewa daima. (Mathayo 12:22-32 na Luka 11:14-23 huandika pia habari hii.
Yesu anaongea vilevile juu ya kumkufuru Roho Mtakatifu kwenye Injili ya Luka;


Luka 12:10  Na kila mtu atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali aliyemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.

Msamaha unatokana na mzizi wa  neno la Kiyunani "aphiemi" linalomaanisha kuondoa au kupuuza. Haimaanishi Mungu husahau dhambi zetu, bali hafikirii tena dhambi zetu na akishatusamehe wokovu wetu unabaki palepale. 

Kufuru ni neno linatokana na Kiyunani "blasphemia" ikimaanisha maneno yasiyo na heshima, kupinga mamlaka ya Mungu. Ni dhamira ya kutomheshimu Mungu. Yesu alipojiita mwana wa Mungu waandishi na Mafarisayo waliona ni kufuru. Katika sheria ya Musa kufuru kwa Mungu adhabu yake ilikuwa kifo (Law 24:10-16)

Mathayo anatumia lugha tofauti. Yeye hasemi "dhambi zote..." bali anasema "yeyote..."


Mathayo 12:32  Naye mtu ye yote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao.


Wote wawili yaani Mathayo na Marko wako sawa, katika ujumbe wa msamaha juu ya Roho Mtakatifu.

Tafakuri;
Kwa nini Yesu anaondoa kufuru  ya Roho Mtakatifu katika msamaha? 
Nafikiri sababu ni kuwa kumkufuru Roho Mtakatifu humuweka mtu mbali na toba, hivyo kuwa mbali na msamaha. 
Mstari wa 29 hauachani na ule wa 28, maana Yesu hasemi kufuru zote mtakazotubu mtasamehewa labda ile ya Roho Mtakatifu, bali anasema kufuru zote mtasamehewa, bali atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa maana atakuwa mbali na toba (Soma tena).

Kwa nini dhambi hii haisameheki?
Kwa nini kumkufuru Baba au Mwana ni msamaha na siyo Roho Mtakatifu?
Baba alipanga ukombozi wa mwanadamu, Mwana akaukamilisha. Ukombozi huu tunaupata tukitubu dhambi na kurejea kwa Kristo. Ni kazi ya Roho Mtakatifu kukamilisha kazi ya Baba na Mwana mioyoni mwetu. Ni kazi ya Roho Mtakatifu kutufungua macho (fahamu) yetu kutuongoza kutubu na kutupa yote aliyopanga Baba, tukapewa na Mwana.

Tukimkufuru na kumkataa Baba na Mwana, bado lipo tumaini kwa Roho Mtakatifu kutuongoza kutubu. Lakini tukiikataa kazi ya Roho Mtakatifu tunajiondoa kwake atuongozaye kutubu, hivyo kujiondolea msamaha wenyewe. 

Hadi hapo naweza kusema hivi;
"Dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu isiyo na msamaha ni tendo la kumkataa, linalomfanya "duni" Roho Mtakatifu  hivyo  kutomwezesha mtu kutubu na kusamehewa"

Kwa maana hiyo tunaalikwa kukataa dhambi katika hali yoyote ili tusitumbukie katika dhambi hii. Tukatae mazingira yoyote ya dhambi kama Yesu alivyosema;


Marko 9:43  Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika;

Roho Mtakatifu ni mtakasaji wa  mioyo yetu. Kumkataa mtakasaji ni kukosa msamaha, jambo ambalo ni hatari sana kwa mkristo. Wataki Yesu anaanza kazi yake alisema;


Mathayo 4:17  Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.


Hivyo maisha ya toba ni agizo. Tusivunje agizo hili kwa kumkataa Roho Mtakatifu ili tuwe na mwisho mwema.


Bwana akubariki.