Date: 
13-03-2023
Reading: 
Isaya 64:6-12

Hii ni Kwaresma;

Jumatatu asubuhi 13.03.2023

Isaya 64:6-12

6 Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo.

7 Tena hapana aliitiaye jina lako, ajitahidiye akushike; kwa kuwa umetuficha uso wako, nawe umetukomesha kwa njia ya maovu yetu.

8 Lakini sasa, Ee Bwana, wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu; sisi sote tu kazi ya mikono yako.

9 Ee Bwana, usione hasira nyingi, wala usiukumbuke uovu siku zote; tazama, angalia, twakusihi, sisi sote tu watu wako.

10 Miji yako mitakatifu imekuwa jangwa, Sayuni umekuwa jangwa, Yerusalemu umekuwa ukiwa.

11 Nyumba yetu takatifu, nzuri, walimokusifu baba zetu, imeteketea moto; vitu vyetu vyote vyenye kupendeza vimeharibika.

12 Utajizuia usiyaangalie mambo haya, Ee Bwana? Utanyamaza, na kututesa sana?

Tutunze mazingira;

Nabii Isaya analeta ujumbe kuwa sisi sote tu kazi ya mikono ya Mungu (8), yaani tumeumbwa na Mungu. Isaya anaweka wazi kuwa dunia tunayoishi pia imeumbwa na Mungu. Lakini Nabii Isaya anaonesha jinsi ambavyo watu hawakutimiza wajibu wao, juu ya uso wa dunia, kwamba watu wote wanastahili rehema ya Mungu. Isaya anaomba huruma ya Mungu kwa ajili ya watu ambao hawakutimiza wajibu wao katika nchi aliyowapa.

Tunakumbushwa kuwa tumeumbwa na Mungu kwa mfano wake, akatupa dunia tuishi na kuitunza. Tusipoitunza dunia tunaharibu uumbaji, hivyo tunatenda dhambi. Yaani tusipotunza mazingira tunaharibu uumbaji, tunatenda dhambi. Tunawajibika kutunza mazingira ili dunia iwe sehemu salama kwa ajili yetu na viumbe vingine vyote.

Tunza mazingira 

Uwe na wiki njema ukitunza mazingira 

 

Heri Buberwa