Date: 
05-01-2023
Reading: 
Isaya 60:17-22

Alhamisi asubuhi tarehe 05.01.2022

Isaya 60:17-22

[17]Badala ya shaba nitaleta dhahabu, 

Na badala; ya chuma nitaleta fedha, 

Na badala ya mti, shaba, 

Na badala ya mawe, chuma; 

Tena nitawafanya wasimamizi wako wawe amani, 

Na hao wakutozao fedha kuwa haki.

[18]Jeuri haitasikiwa tena katika nchi yako, 

Ukiwa na uharibifu hazitakuwa mipakani mwako; 

Bali utaziita kuta zako, Wokovu, 

Na malango yako, Sifa.

[19]Jua halitakuwa nuru yako tena wakati wa mchana, 

Wala mwezi hautakupa nuru kwa mwangaza wake; 

Bali BWANA atakuwa nuru ya milele kwako, 

Na Mungu wako atakuwa utukufu wako.

[20]Jua lako halitashuka tena, 

Wala mwezi wako hautajitenga; 

Kwa kuwa BWANA mwenyewe atakuwa nuru yako ya milele; 

Na siku za kuomboleza kwako zitakoma.

[21]Watu wako nao watakuwa wenye haki wote, 

Nao watairithi nchi milele; 

Chipukizi nililolipanda mimi mwenyewe, 

Kazi ya mikono yangu mwenyewe, 

Ili mimi nitukuzwe.

[22]Mdogo atakuwa elfu, 

Na mnyonge atakuwa taifa hodari; 

Mimi, BWANA, nitayahimiza hayo wakati wake.

Anza yote katika jina la Yesu Kristo;

Ni baada ya Israeli kutoka uhamishoni, Bwana alitoa ahadi ya kuendelea kuwa Mungu wao. Bwana aliwaahidi ulinzi na wokovu. Yeye Bwana pia aliahidi kuendelea kuwa nuru yao. Bwana alikuwa nuru yao ndiyo maana aliwatoa uhamishoni, lakini ahadi hapa ni kuwa nuru haitakoma. Israeli walihakikishiwa kuirithi nchi milele. 

Bwana amekuwa nuru yetu, ndiyo maana tumeumaliza mwaka uliopita na kuuingia mwaka huu. Mungu anatekeleza kwa vitendo ahadi ya kutulinda na kutubariki. 

Kwa nini tuiache neema hii? Neema ya kumpokea Yesu Kristo ambaye amekuwa nasi? Tena yuko nasi na ameahidi kuwa nasi siku zote? Tukimtegemea Yesu tutakuwa na mwaka wenye furaha na mafanikio.

Alhamisi njema.