Date: 
18-02-2023
Reading: 
Zaburi 119:153-160

Jumamosi asubuhi tarehe 18.02.2023

Zaburi 119:153-160

153 Uyaangalie mateso yangu, uniokoe, Maana sikuisahau sheria yako.

154 Unitetee na kunikomboa, Unihuishe sawasawa na ahadi yako.

155 Wokovu u mbali na wasio haki, Kwa maana hawajifunzi amri zako.

156 Ee Bwana, rehema zako ni nyingi, Unihuishe sawasawa na hukumu zako.

157 Wanaonifuatia na watesi wangu ni wengi, Lakini sikujiepusha na shuhuda zako.

158 Nimewaona watendao uhaini nikachukizwa, Kwa sababu hawakulitii neno lako.

159 Uangalie niyapendavyo mausia yako, Ee Bwana, unihuishe sawasawa na fadhili zako.

160 Jumla ya neno lako ni kweli, Na kila hukumu ya haki yako ni ya milele.

Neno lako lina nguvu;

Asubuhi ya leo tunaamshwa na muimbaji wa Zaburi ambaye anaonekana kumuita Bwana amuokoe na mateso aliyokuwa akipitia kwa sababu ya kuifuata sheria ya Bwana. Anakiri kuupata wokovu na kuwa shuhuda mwema katika Bwana. Anayapenda sana mausia ya Bwana, akikazia kuwa neno la Bwana ni kweli, na hukumu zake ni za milele.

Hapa tunapata ujumbe wa kusimama katika neno la Bwana katika hali zote. Changamoto katika maisha tunayoishi haziepukiki. Lakini katikati ya changamoto hizo Yesu anatualika kusimama katika neno lake, na anatuhakikishia ushindi, maana neno lake ni kweli na hukumu yake ya haki ni ya milele.

Jumamosi njema.

Heri Buberwa