Date: 
15-04-2022
Reading: 
Yohana 19:1-7

Hii ni Ijumaa Kuu;

Ijumaa ya tarehe 15.04.2022

Siku ya kukumbuka kufa kwa Yesu;

Masomo;

Zab 22:12-28

Ebr 10:1-7

*Yoh 19:1-7

Yohana 19:1-7

1 Basi ndipo Pilato alipomtwaa Yesu, akampiga mijeledi.

2 Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika vazi la zambarau.

3 Wakawa wakimwendea, wakisema, Salamu! Mfalme wa Wayahudi! Wakampiga makofi.

4 Kisha Pilato akatokea tena nje, akawaambia, Mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yo yote kwake.

5 Ndipo Yesu alipotoka nje, naye amevaa ile taji ya miiba, na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia, Tazama, mtu huyu!

6 Basi wale wakuu wa makuhani na watumishi wao walipomwona, walipiga kelele wakisema, Msulibishe! Msulibishe! Pilato akawaambia, Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe; kwa maana mimi sioni hatia kwake.

7 Wayahudi wakamjibu, Sisi tunayo sheria, na kwa sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.

Aliteswa na kufa kwa ajili yetu;

Kesi ya Yesu imebaki kwenye historia kuwa ya kipekee kwenye historia kwa sababu kubwa ambayo ni mashataka kuwa tofauti toka ngazi ya mahakama moja na nyingine. Kwa ngazi moja mashataka yalikuwa ya kidini, na ngazi iliyofuata mashtaka yakawa ya kisiasa.

Alipopelekwa kwa Kayafa kuhani mkuu alishtakiwa kwa kusema;

-Anaweza kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu

-Yeye ni mwana wa Mungu 

Baada ya kushindwa kumtia hatiani, na Kayafa kukosa mamlaka ya kumhukumu, wakampeleka kwa Pilato wakimshtaki kwa;

-Kujiita mfalme

-Kuzuia watu kulipa kodi kwa Kaisari

Kitendo cha mashtaka kutofautiana ni dhahiri kuwa Yesu hakuwa na kosa lolote ambalo lingemtia hatiani. 

Kushtakiwa na kuteswa kwa Yesu kuliambatana na uovu kama ambavyo tunaweza kuona. Fuatana nami;

=Yesu alikamatwa usiku.

Siyo tu kukamatwa usiku, hawakuwa na kibali cha kumkamata. Baada ya kula karamu na wanafunzi wake, akaenda kuomba na wachache ndipo akakamatwa. Kwa nini usiku? Labda walijua umati uliomuamini usingekuwepo, hivyo kumkamata ingekuwa rahisi. Alipelekwa kwa kuhani usiku! Kuhani anasikiliza mashtaka usiku!

Usiku unawakikisha kufanya mambo nje ya utaratibu. Leo nakualika utafakari, kama unafanya kazi kwa kufuata taratibu zilizowekwa. Unatenda haki au unasubiri usiku?

=Yesu alipigwa kabla ya kuhukumiwa.

Alipokamatwa alipigwa, Pilato akaamuru kabisa apigwe mijeledi wakati alimuona bila hatia! Huyu alikuwa mtuhumiwa. Mtuhumiwa huadhibiwa?!

Nyie mliopewa mamlaka kuwasimamia na kuwahudumia watuhumiwa, watendeeni haki, maana hao ni watuhumiwa tu.

=Ushahidi haukupatana;

Marko anaeleza juu ya ushahidi usiopatana;

Marko 14:55-59

55 Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda juu ya Yesu wapate kumwua; wasione.
56 Kwa maana wengi walimshuhudia uongo, walakini ushuhuda wao haukupatana.
57 Hata wengine wakasimama, wakamshuhudia uongo, wakisema,
58 Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono.
59 Wala hata hivi ushuhuda wao haukupatana.

Kama ushahidi haupatani, maana yake ni uongo. Tujifunze kushuhudia ukweli kwa ndugu zetu.

=Wakati Yesu akishtakiwa, inaaminika wataalamu wa sheria hawakushirikishwa. Inaaminika miongoni mwa nguli wa sheria ambao hawakuhusishwa ni Simoni Mkirene (Yohana haandiki kuhusu huyu ndugu). Injili zote isipokuwa Yohana zinaandika kuwa Simon Mkirene alilazimishwa kubeba msalaba wa Yesu. Hawakumualika atoe uzoefu na ushauri wa kisheria, wakamshurutisha kubeba msalaba.

Ipo tabia ya watu wenye uwezo katika eneo husika, kuondolewa au kuhamishwa ofisi husika ikitokea kuna mradi unakuja, maana wataziba maslahi ya wakuu. Huu ni uovu, maana kazi hazifanyiki kwa viwango, kama ambavyo Yesu hakuhukumiwa kwa haki.

=Yesu alihukumiwa kifo;

Hakukuwa na ushahidi wa kumtia Yesu hatiani! Kayafa alikosa cha kufanya, Pilato akaona Yesu hana hatia, lakini akahukumiwa kifo! Hii haikuwa sahihi!

Hapa kila mmoja wetu analo la kujiuliza; tunatenda haki ipasavyo?

Katika yote hayo, leo tumemsoma Pilato ambaye alishindwa kusimama kwa nafasi yake hadi Yesu kuuawa. Najaribu kumsoma Pilato kama ifuatavyo;

1. Pilato alishindwa kusimama kama kiongozi.

Alishindwa kutumia nafasi yake kuzuia uovu. Binafsi nauona huu kama udhaifu. Haiwezekani kiongozi mkubwa ukakosa kuwa na maamuzi. Aliishia kunawa mikono! 

Kwa wewe Kiongozi, huu mfano wa Pilato haukubaliki, hauvumuliki. Kutofanya uamuzi sahihi kunasababisha wasio na hatia kukosa haki yao. Kushindwa kusimamia haki kunasababishavitendo viovu kama rushwa, hatimaye wasio na uwezo kukosa haki yao. Usiwe kama Pilato. 

Simama kwa nafasi yako.

2. Nguvu ya uuma ilimzidi Pilato nguvu.

Nguvu ya umma ilikosa hoja, wakazidi kusema asulubiwe! Pilato naye akaruhusu asulubiwe! Mtu aliyeonekana hana hatia, unaruhusu asulubiwe?! Nguvu ya umma!

Mimi huwa naiita nguvu ya umma "umoja wa uovu". Ni kwa sababu mara nyingi nguvu ya umma huwa haizingatii sheria katika kufanya maamuzi. Huangalia wanataka nini, na kumwadhibu mtu kama hawamtaki. Nguvu ya umma ingefuata sheria, Yesu asingeuawa, maana hakuwahi kutiwa hatiani na mamlaka yoyote. 

Nguvu ya umma ilimtishia Paulo mamlaka yake kwa kumwambia asiporuhusu Yesu kuteswa, siyo rafiki yake Kaisari!

Yohana 19:12-13

12 Na tangu hapo Pilato akatafuta kumfungua; lakini Wayahudi wakapiga makelele wakisema, Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanyaye kuwa mfalme humfitini Kaisari.
13 Basi Pilato, aliposikia maneno hayo, akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo Sakafu ya Mawe, au kwa Kiebrania, Gabatha.

Pamoja na Pilato kutishika, tunaweza kufananisha hali hii na pale tunapotishika na mambo ya dunia tukamwacha Yesu. Kumbe hatutakiwi kuondoka kwa Yesu kamwe.

Mwisho;

Pilato alizidiwa, hadi kutojua afanye nini na Yesu. 

Unafanya nini na Yesu?

Yesu alikataliwa, akateswa na kufa. Ni mfalme aliyekuwa akijitoa kwa ajili ya ulimwengu.

Wewe unafanya nini na Yesu?

Tusiadhimishe Ijumaa kuu kwa historia tu, bali historia itukumbushe kuwa Yesu aliteswa na kufa kwa ajili yetu. Hivyo tubadilike na kumfuata kwa uaminifu, tukimpa maisha yetu sasa na hata milele. Amina.

Hii ni Ijumaa kuu.