Date: 
26-09-2022
Reading: 
Yohana 12:39-43

Jumatatu asubuhi tarehe 26.09.2022

Yohana 12:39-43

[39]Ndiyo sababu wao hawakuweza kusadiki; kwa maana Isaya alisema tena,

[40]Amewapofusha macho, 

Ameifanya mizito mioyo yao; 

Wasije wakaona kwa macho yao, 

Wakafahamu kwa mioyo yao, 

Wakaongoka, nikawaponya.

[41]Maneno hayo aliyasema Isaya, kwa kuwa aliuona utukufu wake, akataja habari zake.

[42]Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi.

[43]Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu.

Uchaguzi wa busara;

Pamoja na Yesu kuhubiri, kufundisha na kuponya, wapo ambao hawakuamini. Ukisoma kabla ya somo la leo asubuhi, Yesu anaeleza habari za kifo chake kwa ajili ya kuukomboa ulimwengu. Lakini bado wapo ambao hawakuamini. Katika somo la asubuhi hii, katika mstari wa 40 Yesu anamrejea nabii Isaya (Isaya sura ya 6) akionesha wasioamini, yaani waliopofuka mioyo yao. 

Yesu anawarejea pia ambao walimwamini lakini wakaogopa kumkiri wasije kutengwa na Mafarisayo kwenye masinagogi. Mafarisayo walipenda Utukufu, hawakumuona Yesu kuwa na Utukufu, hivyo hawakumwamini, wakawa kikwazo pia kwa wengine kumwamini Yesu.

Tabia ya kutokuamini haitakiwi kuwepo kwetu. Wala hatutakiwi kuwa kikwazo kwa wengine kumwamini na kumkiri Yesu. Kuchagua kumfuata Yesu ndiyo uchaguzi wa busara kuliko uchaguzi mwingine wowote. Lakini pia kuwaonesha wengine uchaguzi mzuri ni wajibu wetu, yaani kumhubiri Kristo ili wote wachague kumfuata yeye. Tuhakikishe chaguo letu ni Yesu Kristo.

Nakutakia wiki njema yenye uchaguzi wa busara.