Date: 
04-03-2022
Reading: 
Yeremia 29:1-14

Hii ni Kwaresma;

Ijumaa ya tarehe 04.02.2022, Siku ya maombi ya dunia.

Masomo;
Zab 107:33-43
1 Yoh 4:9-10
*Yer 29:1-14

Yeremia 29:1-14
1 Maneno haya ndiyo maneno ya waraka, ambao nabii Yeremia aliupeleka toka Yerusalemu, kwa hao waliobaki wa wakuu waliochukuliwa mateka, na kwa makuhani, na kwa manabii, na kwa watu wote, ambao Nebukadreza aliwachukua mateka toka Yerusalemu hata Babeli;
2 (hapo walipokwisha kutoka Yerusalemu Yekonia mfalme, na mama yake mfalme, na matowashi, na wakuu wa Yuda na Yerusalemu, na mafundi, na wahunzi;)
3 kwa mkono wa Elasa, mwana wa Shafani, na Gemaria, mwana wa Hilkia, (ambao Sedekia, mfalme wa Yuda, aliwatuma hata Babeli, kwa Nebukadreza, mfalme wa Babeli), kusema,
4 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, awaambia hivi watu wote waliochukuliwa mateka, niliowafanya wachukuliwe toka Yerusalemu mpaka Babeli;
5 Jengeni nyumba, mkakae ndani yake, kapandeni bustani, mkale matunda yake;
6 oeni wake, mkazae wana na binti; kawaozeni wake wana wenu, mkawaoze waume binti zenu, wazae wana na binti; mkaongezeke huko wala msipungue.
7 Kautakieni amani mji ule, ambao nimewafanya mchukuliwe mateka, mkauombee kwa Bwana; kwa maana katika amani yake mji huo ninyi mtapata amani.
8 Maana Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Manabii walio kati yenu, na wabashiri wenu, wasiwadanganye ninyi, wala msisikilize ndoto zenu, mnazootesha.
9 Kwa maana kwa jina langu hutabiri maneno ya uongo kwenu; mimi sikuwatuma, asema Bwana.
10 Maana Bwana asema hivi, Babeli utakapotimiziwa miaka sabini, nitawajilia ninyi, na kulitimiza neno langu jema kwenu, kwa kuwarudisha mahali hapa.
11 Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.
12 Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza.
13 Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.
14 Nami nitaonekana kwenu, asema Bwana, nami nitawarudisha watu wenu waliofungwa, nami nitawakusanya ninyi, nikiwatoa katika mataifa yote, na katika mahali pote, nilikowafukuza, asema Bwana; nami nitawaleta tena, hata mahali ambapo kutoka hapo naliwafanya mchukuliwe mateka.

Tafakari;

Utangulizi;
Yeremia alikuwa nabii wa Mungu aliyefanya kazi yake wakati wa watawala wa mwisho wa Yuda, katika nusu ya kwanza ya karne ya sita KK. Israeli ilikuwa imegawanyika katika falme mbili, Efraimu Kaskazini na Yuda Kusini. Yeremia alitokea Efraimu, lakini Mungu alimtuma katika Yuda kutoa unabii katika Yerusalemu ambao ulikuwa makao makuu, penye kiti cha mfalme na hekalu pia.
Yerusalemu ilikuwa alama muhimu kwa Israeli, hivyo Mungu kumtuma Yeremia kuhubiri pale haikuwa hivi hivi tu. Jambo lingine muhimu ni kuwa alikuwa mgeni katika Yuda. Yeye alitokea Efraimu, lakini akiongozwa na Bwana.

Somo letu ni ujumbe wa Bwana  kwenda kwa Waebrania walioko uhamishoni Babeli. Wakati anapeleka ujumbe huu, Yeremia hakuwa mdogo tena, alikuwa sasa amefanya unabii kwa muda akisema na watu, lakini na wafalme pia.

Ujumbe wa Yeremia;
Yeremia aliwatuhumu kwa kutoifuata sheria ya Mungu; hawakuwajali wajane na yatima na maskini. Hii ilikuwa dalili mbaya kiroho katika nchi, ambapo hali ingeendelea, mwisho wa watu usingekuwa mzuri. 

Kama tulivyoona, utabiri wa Yeremia ulikuwa hukumu juu ya Yuda kwa sababu ya kuyumba kiimani kwa Mungu, Yeremia akiona Babeli kuiongoza Yuda kama adhabu ya Mungu kwa kutokuamini kwao. Yeremia anawasihi wasikilizaji wake kutowaamini manabii wa uongo, maana hawakutumwa na Bwana.

Ni vigumu kudumu katika imani yako ukiwa mbali na kwenu, ukiwa na akili kama za Israeli wakati ule. Lakini Yeremia anawaambia kuwa Mungu wao siyo wa Yerusalemu tu, bali hata Babeli. 
Katika ujumbe wa Yeremia, anatoa changamoto ya mihimi mitatu; ufalme, nchi na hekalu. Yeremia anawaambia kuwa Mungu ni mkuu, aliyeko sehemu zote duniani. Kwamba anaweza kuabudiwa hata Babeli.

Mawazo ya Israeli yalikuwa kwamba suluhisho la matatizo yao ni kurudi Yerusalemu kwenye nchi, hekalu  na ufalme, mahali ambapo palikuwa kiini cha maisha yao ya kidini. Kitendo cha kuwa uhamishoni kilikuwa cha muda tu, na muda huo wangevumilia uishe. Lipo funzo hapa, la uvumilivu katika kungojea mapenzi ya Mungu yatimizwe, kwa utukufu wake.

Maono ya Yeremia ni kuwa Bwana hana mipaka ya eneo, muda na mawazo ya watu katika kutimiza atakayo. Ipo shida Kanisa leo, katika kutafakari mapenzi ya Mungu. Wengi hutaka Mungu atende waonavyo au watakavyo! 

Leo hii, zipo hali tofauti zinazotufanya tujione hatuko sawa, yaani kama tuko uhamishoni vile. Tuko vibaya labda kisiasa, kiuchumi, kazi hakuna, na changamoto nyinginezo. Tunafanyaje kuzikabili? Tunaziona ni za kudumu? 

Yeremia anatupa ujumbe wa tumaini na ahadi kwamba Mungu hatuachi popote tuendapo.  Hili ni neno la tumaini kwa kila kizazi. Hii ni kwa sababu kwa namna fulani kila mmoja kuna mahali anaweza kuwa hayuko sawa. Tuko safarini, tukielekea nyumbani. Katika waraka wa Waebrania Mungu anasema nasi;
Waebrania 13:14  Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao.

Popote uendapo, lolote litokealo kwako, Mungu anakuhakikishia kuwa na wewe. Uwe nyumbani, au mbali. Uwe mzima au kifoni. 
Bwana yu nawe.
Utukufu kwa Yesu!