Date: 
03-08-2022
Reading: 
Wakolosai 1:9-12

Jumatano asubuhi tarehe 03.08.2022

Wakolosai 1:9-12

[9]Kwa sababu hiyo sisi nasi, tangu siku ile tuliposikia, hatuachi kufanya maombi na dua kwa ajili yenu, ili mjazwe maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni;

[10]mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya Mungu;

[11]mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake, mpate kuwa na saburi ya kila namna na uvumilivu pamoja na furaha;

[12]mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru.

Mungu amejaa neema inayotuwezesha;

Mtume Paulo anamshukuru Mungu kwa ajili ya Wakolosai pale alipoona wanaendelea vizuri katika Kristo. Katika shukrani yake hiyo anawaombea wawe na maarifa katika Kristo ili wadumu katika kufanya yaliyo mapenzi ya Mungu wakizaa matunda yapasayo katika Bwana. Anawaombea uvumilivu, furaha na maisha ya ushuhuda katika Kristo siku zote.

Sala hii ya Mtume Paulo inatutuma kutafakari kama tunadumu katika neema ya Mungu, tukijawa na maarifa katika yeye (Kristo). Tunaalikwa kutafakari kama maisha yetu yanaakisi kuzaa matunda mema kama tunavyoagizwa na Yesu Kristo, maana tutatoa hesabu ya uwakili wetu katika tutendayo. Katika yote, tunakumbushwa kufanya yote kwa jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, maana katika yeye tunayo neema inayotuwezesha.

Siku njema