Date: 
24-09-2022
Reading: 
Waefeso 5:15-21

Jumamosi asubuhi tarehe 24.09.2022

Waefeso 5:15-21

[15]Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima;

[16]mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu.

[17]Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana.

[18]Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho;

[19]mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu;

[20]na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo;

[21]hali mnanyenyekeana katika kicho cha Kristo.

Uwakili wetu kwa Mungu;

Mtume Paulo anawaandikia Waefeso kuepuka kuishi kama wasioamini. Katika hili anawaambia wawe na hekima itokayo kwa Kristo wakiuepuka uovu. Anawasihi kutokuwa wajinga, bali wafanye yaliyo mapenzi ya Mungu kwa uongozi wa Roho Mtakatifu. Katika yote anawasisitizia kumshukuru Mungu kwa ajili ya baraka zake.

Tutafakari njia zetu kama tunaishi na kuenenda kwa hekima kwa uongozi wa Roho Mtakatifu. Hekima ya Mungu ndiyo hutusaidia kufanya maamuzi sahihi, yaani ni kwa jinsi gani tuishi kwa kumfuata Kristo. Tukimfuata Kristo tusisahau kumwabudu na kumtolea kwa shukrani, maana katika yeye sisi tumeokolewa.

Uwe na Jumamosi njema