Date: 
06-02-2023
Reading: 
Waamuzi 10:6-16

Jumatatu asubuhi tarehe 06.02.2023

Waamuzi 10:6-16

6 Kisha wana wa Israeli walifanya tena yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana, wakawatumikia Mabaali, na Maashtorethi, na miungu ya Shamu, na miungu ya Sidoni, na miungu ya Moabu, na miungu ya wana wa Amoni, na miungu ya Wafilisti; nao wakamwacha Bwana, wala hawakumtumikia yeye.

7 Hasira za Bwana ziliwaka juu ya Israeli, akawauza na kuwaua mikononi mwa Wafilisti, na mikononi mwa wana wa Amoni.

8 Nao wakawasumbua na kuwaonea wana wa Israeli mwaka huo; waliwaonea wana wa Israeli wote waliokuwa ng'ambo ya pili ya Yordani katika nchi ya Waamori, iliyoko huko Gileadi, muda wa miaka kumi na minane.

9 Wana wa Amoni nao wakavuka Yordani ili wapigane na Yuda, na kupigana na Benyamini, na nyumba ya Efraimu; basi hivyo Israeli walikuwa wanasumbuliwa sana.

10 Ndipo wana wa Israeli wakamlilia Bwana, wakisema, Sisi tumekufanyia dhambi, kwa sababu tumemwacha Mungu wetu, na kuyatumikia Mabaali.

11 Naye Bwana akawaambia wana wa Israeli, Je! Sikuwaokoa ninyi na hao Wamisri, na Waamori, na wana wa Amoni, na Wafilisti?

12 Hao Wasidoni nao, na Waamaleki, na Wamaoni, waliwaonea, nanyi mlinililia, nami niliwaokoa na mikono yao.

13 Lakini mmeniacha mimi, na kuitumikia miungu mingine; basi kwa ajili ya hayo mimi sitawaokoa tena.

14 Haya, endeni mkaililie hiyo miungu mliyoichagua; na hiyo iwaokoe wakati wa kusumbuka kwenu.

15 Wana wa Israeli wakamwambia Bwana Tumefanya dhambi; utufanyie yote uyaonayo kuwa ni mema; lakini tuokoe, twakusihi, siku hii ya leo, haya tu.

16 Nao wakaiondoa hiyo miungu ya kigeni iliyokuwa kati yao, nao wakamtumikia Bwana; na roho yake ilihuzunika kwa sababu ya msiba wa Israeli.

Tunaokolewa kwa neema;

Wana wa Israeli walimkosea Mungu, naye Mungu alichukia akawaacha. Baada ya kuachwa walipata shida sana maana waliteswa sana na Wafilisti, na wana wa Amoni. Baada ya mateso mengi walimlilia Bwana wakiomba msamaha wa dhambi, wakikiri kuwatumikia Mabaali. Walitambua kumkosea Mungu, wakawa tayari kufanya toba.

Israeli hawakukumbuka Bwana alivyowatoa Misri, ndiyo maana tumeona Bwana akisema sitawaokoa tena. Ukisoma sura ya 11, unaona Israeli wakishinda vita, yaani Bwana alikuwa upande wao.

Neema ya Mungu ilikuwa kwao baada ya kutubu. Tukitubu dhambi zetu Bwana hutusamehe na kututenga na uovu. Tutambue kuwa Bwana ametuokoa ili tumtumikie na kumwabudu yeye peke yake. Utukufu una yeye Bwana, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Tunaokolewa kwa neema.

Uwe na wiki njema yenye ushuhuda.

 

Heri Buberwa