Event Date: 
31-10-2020

Waalimu wa shule ya Jumapili ya Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront, hivi karibuni walihudhuria semina iliyoandaliwa na usharika na kufanyika siku ya Jumamosi tarehe 31/10/2020. Semina hiyo ilishirikisha walimu wa usharikani pamoja na walimu wa Shule za Jumapili kutoka katika mitaa inayotunzwa na Usharika wa Kanisa Kuu, mitaa hiyo ni pamoja na Viwege, Dondwe, Mvuti na Tabora.

Lengo la semina hiyo lilikuwa ni kuwajengea walimu hao uwezo wa kufundisha, kuwaelimisha juu ya mbinu mbalimbali za kufundishia pamoja na kuwaelimisha njia za wao kujitambua kama watumishi wa Mungu.

Mchungaji Joseph Mlaki akitoa somo katika semina ya walimu wa Shule ya Jumapili, Usharikani Azaniafront.

Masomo makuu yaliyofundishwa siku hiyo yalikuwa ni ‘maisha ya mwalimu wa watoto wa Shule ya Jumapili’, somo ambalo lilifundishwa na Mwl Albano Fernando. Somo jingine lilikuwa ni juu ya mbinu za ufundishaji, na lilifundishwa na Mwl Rodric Natai. Pia kulikuwa na somo la mwongozo wa ufundishaji wa Shule ya Jumapili lililofundishwa na Mchungaji Joseph Mlaki.

 Walimu wa Shule ya Jumapili wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuhudhuria semina iliyofanyika Usharikani, Azaniafront.

Walimu wa Shule ya Jumapili wakitunza kumbukumbu wakati wa semina iliyofanyika ili kuwaongezea ujuzi

Mchungaji Gwakisa Mwaipopo (katikati) akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina kwa ajili ya walimu wa Shule ya Jumapili, Usharikani Azaniafront.

Semina hiyo iliyohudhuriwa kwa wingi na walimu wa madarasa yote ya Shule ya Jumapili, ilipata baraka za kufunguliwa na Mchungaji Gwakisa Mwaipopo.

 

Habari na Picha vimekusanywa na Jane Mhina