Event Date: 
21-10-2022

Kama ilivyoainishwa katika kalenda ya KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Jumapili ya tarehe 2 Oktoba 2022 Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral uliadhimisha Sikukuu ya Mikael na Watoto.

Sikukuu ya Mikael na watoto hufanyika kila mwaka kwa ajili ya kumkumbuka malaika Mikel na watakatifu wote pamoja na watoto. Ibada hii hufanyika kwa kuongozwa na watoto wakisaidiana na walimu wao pamoja na mtumishi wa usharika (parish worker).

Kwa mwaka wa 2022, Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront zilifanyika ibada tatu kuadhimisha sikukuu hiyo, ibada za Kiswahili mbili na moja ya Kiingereza. Katika ibada zote tatu watoto walipata fursa ya kuongoza shughuli zote za ibada ikiwemo kusoma litrugia, matangazo pamoja na kuongoza sala.

Akihubiri katika ibada za Kiswahili, Mwalimu Magdalena Kivulenge aliwaasa washarika, wazazi pamoja na walezi kuwapenda watoto na kuwatimizia mahitaji yote muhimu ikiwa ni pamoja na kuwalea katika misingi ya neno la Mungu “Kuna kasumba kwamba watoto wa siku hizi hawafundishiki, hawapendi kuonywa wala kujifunza, lakini sisi kama wakristo tumepewa wajibu wa kuwafundisha hawa watoto kuwajibika na kufanya kazi. Tumwombe Mungu atusaidie kutimiza huu wajibu”, alisema.

Usimwonee huruma mtoto kwamba hii kazi ni ya dada wa kazi au kazi ya mwalimu wake, hapana, huu ni wajibu wetu kama wazazi au walezi kuhakikisha watoto wetu wanafuata mafundisho yaliyo sahihi. Tumepewa wajibu, tumwombe Mungu atusaidie kutimiza huo wajibu wetu kwa watoto wetu ili tupate dhawabu,” Bi Magdalena aliongeza.

Baadhi ya Walimu wa Shule ya Jumapili ( English + Swahili) katika picha ya pamoja.

Pia katika ibada zote tatu watoto walipata fursa ya kusema mistari ya moyo, kufanya ngonjera na kuimba nyimbo mbalimbali. Vyote hivyo vilibeba ujumbe kwa wazazi kuhusu kuwalea watoto vyema ili wakue katika maadili mema ya kikristo.

Kwa upande wake, Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front, Mchungaji Charles Mzinga, aliwashukuru washarika wote, walimu pamoja na wanafunzi wa shule ya Jumapili kwa kuwezesha kufanyika kwa sikukuu hiyo ambayo ni muhimu katika kuandaa kizazi bora kinachomtumikia Yesu Kristo.

Mara baada ya ibada zote tatu watoto walipata fursa ya kukusanyika kwa pamoja na kushriki katika michezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukata keki.

Matukio katika Picha

Watoto wakijumuika katika michezo mbalimbali iliyofanyika siku hiyo.

Watoto wakijumuika katika michezo mbalimbali iliyofanyika siku hiyo.

Keki kwa ajili ya Sikukuu ya Mikael na Watoto pia ilikuwepo 

Sehemu ya watoto wa shule ya Jumapili/ Sunday School wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ibada.