Date: 
02-08-2022
Reading: 
Tito 3:1-11

Jumanne asubuhi tarehe 02.08.2022

Tito 3:1-11

[1]Uwakumbushe watu kunyenyekea kwa wenye uwezo na mamlaka, na kutii, na kuwa tayari kwa kila kazi njema;

[2]wasimtukane mtu ye yote, wasiwe wagomvi, wawe wema, wakionyesha upole wote kwa watu wote.

[3]Maana hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili, tulikuwa waasi, tumedanganywa, huku tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi, tukiishi katika uovu na husuda, tukichukiza na kuchukiana.

[4]Lakini wema wake Mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa;

[5]si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu;

[6]ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu;

[7]ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu.

[8]Ni neno la kuaminiwa; na mambo hayo nataka uyanene kwa nguvu, ili wale waliomwamini Mungu wakumbuke kudumu katika matendo mema. Hayo ni mazuri, tena yana faida kwa wanadamu.

[9]Lakini maswali ya upuzi ujiepushe nayo, na nasaba, na magomvi, na mashindano ya sheria. Kwa kuwa hayana faida, tena hayana maana.

[10]Mtu aliye mzushi, baada ya kumwonya mara ya kwanza na mara ya pili, mkatae;

[11]ukijua ya kuwa mtu kama huyo amepotoka, tena atenda dhambi, maana amejihukumu hatia yeye mwenyewe.

Mungu amejaa neema inayotuwezesha;

Mtume Paulo anamwandikia Tito awakumbushe watu kudumu katika kutenda mema. Tito anaambiwa kuhubiri unyenyekevu, upendo, utu wema na upole. Paulo anapomtuma Tito anaangazia kuacha maisha ya zamani yaliyojaa kutokuwa na akili, uasi, anasa na uovu wa kila aina. Lakini wokovu ulikuja kwa njia ya kifo cha Yesu msalabani, na siyo kwa kustahili kwetu, bali kwa neema ya Mungu.

Ujumbe wa Mtume Paulo kwa Tito ni kulikumbusha Kanisa kuacha maisha ya zamani, na kuishi maisha mapya katika Kristo. Maisha mapya ni pale tunapoishi kwa kuacha mambo yasiyompendeza Mungu, tukifanya toba wakati wote. Tujiepushe na uovu maana haufai, hauna maana, hauna faida. Neema ya Mungu yatosha. 

Siku njema.