"Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie kwa maana ufalme wa mbingu ni wao", hayo ni maneno ya kutoka katika Biblia yaliyotumika katika mahubiri yaliyofanyika katika ibada ya sikukuu ya Mikael na watoto iliyofanyika siku ya Jumapili tarehe 27 September 2020 katika Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront.
Sikukuu ya Mikael na watoto, hufanyika kila mwaka kwa ajili ya kumkumbuka malaika Mikel na watakatifu wote pamoja na watoto. Ibada hii hufanyika kwa kuongozwa na watoto wakisaidiana na walimu wao pamoja na mtumishi wa usharika (parish worker).
Kwa mwaka wa 2020, Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront zilifanyika ibada mbili kuadhimisha sikukuu hiyo, ibada ya kiswahili na kiingereza. Watoto na waalimu kutoka ibada zote mbili waliendesha ibada hizo kwa kuongoza kusoma litrugia, kutoa mahubiri, nyimbo n ahata kusoma matangazo ya usharika.
Katika ibada ya Kiswahili, litrugia ilisomwa na mtoto Morine Mwakilembe, matangazo yalisomwa na mtoto Ethan Kakolaki na mahubiri yaliongozwa na mwalimu Magdalena Kivulenge. Pia katika ibada ya Kiingereza, litrugia ilisomwa na mtoto Ellie Thompson na mahubiri yaliongozwa na mwalimu Kenny Sinare.
13 Basi wakamletea watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. 14 Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. 15 Amin, nawaambieni, Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. 16 Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia.
Akihubiri katika ibada ya Kiswahili, Mwalimu Magdalena Kivulenge aliwaasa washarika kuwapenda watoto na kuwatimizia mahitaji yote muhimu. “Kama wazazi tunawajibika kuwalea na kuwapa matunzo bora watoto wetu kwa kuwapa mahitaji muhimu ambayo yanagusa kimwili, kiakili na kiroho”, alisema Mwalimu Magdalena.
Walimu wa Shule ya Jumapili wakiwasalimu washarika katika ibada ilyofanyika Usharikani kuadhimisha sikukuu ya Mikael na Watoto.
Pia katika ibada zote mbili watoto walipata fursa ya kusema mistari ya moyo, kufanya ngonjera na kuimba nyimbo. Vyote hivyo vilibeba ujumbe kwa wazazi kuhusu kuwalea watoto vYema ili wakue katika maadili mema ya kikristo.
Kwa upande wake, Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront, Mchungaji Charles Mzinga, aliwashukuru washarika wote, walimu pamoja na wanafunzi wa shule ya Jumapili kwa kuwezesha kufanyika kwa sikukuu hiyo ambayo ni muhimu katika kuandaa kizazi bora kinachomtumikia Yesu Kristo.
Katika ibada zote mbili watoto wapatao 250 walishiriki na walipewa zawadi mbalimbali kutoka kwa uongozi wa Usharika.
Mchungaji Charles Mzinga akikabidhi zawadi ya shukrani kwa Jane Mhina, mmoja wa walimu wa Shule ya Jumapili ya Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront.
Wazazi na walezi wakifurahia namna watoto wa Shule ya Jumapili wanavyoendesha ibada kanisani katika sikukuu ya Mikael na Watoto.
Watoto wakitoa burudani ya nyimbo za injili katika kuadhimisha sikukuu ya Mikael na Watoto katika Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront.
Kuona picha zaidi, tembelea: https://drive.google.com/drive/folders/1Fs1ZWBssSdkDg2Rz640XSyzNVLtfR1AZ...